Friday, December 19, 2025
spot_img
HomeBiasharaSerikali yashauriwa kutambua thamani ya Green Garnet kufuatia ongezeko la mahitaji duniani

Serikali yashauriwa kutambua thamani ya Green Garnet kufuatia ongezeko la mahitaji duniani

●Green Garnet ya Tanzania Inaongoza kwa Ubora Duniani.

●Ina sifa ya uzito wa kuanzia graviti ya 3.5 hadi 4.3.

📍Simanjiro – Manyara

Wadau Simanjiro waiomba Serikali  kuyatambua rasmi madini ya Green Garnet kama miongoni mwa madini yenye thamani kubwa, kufuatia ongezeko la mahitaji ya madini hayo katika soko la kimataifa kutokana na uwepo wake kwa wingi katika baadhi ya maeneo ya nchi.

Ushauri huo ulitolewa katika Mikoa ya Arusha na Manyara kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wa madini vito, waongezaji thamani , wachimbaji na  wamiliki wa leseni za uchimbaji ,  wakieleza kuwa madini ya Green Garnet (Tsavorite) yana thamani kubwa duniani lakini bado hayajapewa uzito unaostahili katika mifumo ya kisheria na kibiashara nchini.

Mwenyekiti wa Wachimbaji wa Tanzanite mkoani Manyara Money Kassanga alisema, kutokana na kutokuwapo kwa tathmini rasmi ya thamani ya madini hayo , wengi wao huuza mawe hayo kwa bei ya chini isiyoakisi thamani halisi ya soko la kimataifa jambo linalopelekea kushusha thamani ya madini haya kuanzia kwa mchimbaji mpaka mfanyabiashara.

Kassanga aliongeza kuwa , kuwepo kwa hali hiyo imekuwa ikiwakosesha mapato stahiki na kupunguza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.

“Mara nyingi tunachimba bila kujua thamani kamili ya mawe tunayopata. Kukosekana kwa taarifa rasmi za kimfumo na miongozo  ndani ya nchi kunasababisha  madalali kununua madini kwa bei ndogo sana kutoka kwa mchimbaji,” alisema Kassanga

Kwa upande wake mfanyabiashara wa madini ya vito mkoani Arusha, Peter Pereira alieleza kuwa, Tanzania ina madini ya vito aina mbalimbali yakiwemo madini green garnet (Tsavorite) ambayo kwasasa yanatambulika kama moja ya madini yenye thamani kubwa katika soko la kimataifa, hivyo Serikali kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini waweke mikakati shirikishi itakayotambua na kuyaweka  madini haya katika taswira ya kipekee.

Pereirra aliongeza kuwa , changamoto kubwa inayopelekea  kushuka kwa thamani ya madini kama haya ni utoroshwaji na uuzaji kwa njia zisizo halali, hivyo mamlaka husika zichukue hatua za haraka ili kutunza thamani ya madini haya.

Mthaminishaji wa madini ya vito kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mirerani Seleman Ismael  alieleza kuwa, madini ya Green Garnet ni moja ya  jiwe la thamani linalotumika zaidi katika utengenezaji wa vito vya thamani (jewellery) na linatajwa kuwa miongoni mwa vito vinavyopendwa zaidi katika masoko ya Ulaya, Asia na Marekani kutokana na rangi yake ya kijani yenye mvuto mzuri pamoja ugumu wake unaopelekea kuwa imara wakati wa kuongezewa thamani , ubora wa sifa hizo kwa green garnet ndiyo zinatofautisha na madini mengine ya vito yakiwemo madini ya Tanzanite.

Akielezea kuhusu sifa za madini ya Green garnet, alieleza kuwa green garnet ina uzito wa graviti ya kuanzia kipimo cha 3.5 hadi 4.3 na kwa upande wa ugumu ina kipimo cha ugumu aina ya Mohs ya kuanzia 6.5 hadi 7.5.

Madini ya Green Garnet aina ya Tsavorite nchini Tanzania inahusiana kwa karibu na ugunduzi wa madini ya vito Afrika Mashariki kuanzia nusu ya pili ya karne ya 20.

Nchini Tanzania madini ya Green garnet  yaligunduliwa rasmi  kaskazini mwa Tanzania mwanzoni mwa miaka ya 1970.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments