Serikali imetoa uamuzi wa mwisho kuhusu umiliki wa mashamba yaliyokuwa na mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na mwekezaji wa Kampuni ya Transcontinental katika eneo la Kikongo, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani.
Akisoma maelekezo ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa wananchi Desemba 17, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema maamuzi hayo yametokana na kazi ya tume maalum iliyoundwa kuchunguza mgogoro huo, ambayo imekamilisha uchunguzi wake.
Kunenge amesema kuwa, kwa mujibu wa maelekezo ya Waziri wa Ardhi, shamba namba 9 la Lupunga limebainika kuwa ni mali halali ya Tariq Ahmed, aliyemilikishwa shamba hilo mwaka 1987. Ameeleza kuwa wananchi wote wanaoendesha shughuli ndani ya shamba hilo hawana uhalali wa kisheria.
Kuhusu shamba namba 30/1 lililopo maeneo ya Chekereni na Lupunga lenye ukubwa wa hekta 1,082.4, Kunenge amesema kulikuwepo mgogoro kati ya Kampuni ya Transcontinental na baadhi ya wananchi waliodai kulipwa fidia wakidai kuwa wao ni wamiliki wa asili wa eneo hilo.


Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya tume, hati ya umiliki wa shamba hilo haijawahi kubatilishwa tangu lilipomilikishwa kwa kampuni hiyo mwaka 1987 kwa muda wa miaka 99. Kutokana na uchunguzi huo, Waziri wa Ardhi ameamua kuwa mmiliki halali wa shamba namba 30/1 ni Kampuni ya Transcontinental na kwamba iendelee na shughuli zake za uwekezaji kwa mujibu wa makubaliano yake na Serikali.
Kunenge amesema kuwa wote walioingia ndani ya shamba hilo bila idhini wameingia kinyume cha taratibu na sheria, hivyo wanatambuliwa kama wavamizi. Aidha, Waziri wa Ardhi ameridhia wananchi 214 kupewa kila mmoja eneo la mita za mraba 500 kwa ajili ya ujenzi wa makazi, ambapo gharama za upimaji zitagharamiwa na kampuni husika, huku wananchi wakigharamia umiliki.
Tume hiyo pia ilibaini kuwa madai ya fidia hayakuwa na msingi wa kisheria, kwani shamba hilo lilikuwa tayari limemilikishwa kwa kampuni, na wananchi waliondolewa katika eneo hilo wakati wa Operesheni Vijiji, huku wakirejea baadaye mmoja mmoja kwa shughuli ndogo kama kuokota korosho na kuni.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Pwani amezielekeza halmashauri zote mkoani humo kuzingatia kikamilifu mwongozo wa utoaji wa vibali vya ujenzi. Pia amewaagiza viongozi wa Serikali za mitaa kuacha kujihusisha na masuala ya uuzaji wa ardhi, akieleza kuwa baadhi yao wamekuwa chanzo cha migogoro ya ardhi.
Kwa upande wake, Tariq Ahmed ameishukuru Serikali kwa kumaliza mgogoro huo, akisema kuwa ulikuwa ukikwamisha utekelezaji wa shughuli za uwekezaji katika eneo hilo.






