Zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi waliopisha Mradi wa Gridi Imara limezinduliwa rasmi katika maeneo ya Mkata, Handeni na Kilindi, ambapo serikali imeahidi kulinda maslahi ya wananchi na kuhakikisha huduma ya nishati bora inawanufaisha wote.
Akizindua zoezi hilo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, alisema kiasi cha Sh. bilioni 1.3 kimetengwa kwa ajili ya malipo ya fidia, hatua aliyoitaja kuwa ni kielelezo cha kuthamini utu na mchango wa wananchi waliopisha mradi huo.
“Fidia hii ni kielelezo cha kujali utu na uwekezaji wa kila mmoja. Jukumu la wananchi sasa ni kulinda miundombinu ya umeme ili manufaa ya mradi huu yaendelee kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo. Tukiharibu au kutoheshimu miundombinu hii, hasara kubwa itakuwa yetu sote,” alisema Nyamwese.


Kwa upande wake, Meneja wa Mradi, Mhandisi Jafari Mpina, alisema serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mfumo wa umeme katika Wilaya ya Handeni, hatua itakayochochea fursa za kiuchumi kwa wananchi, ikiwemo kuimarisha biashara na kuongeza ajira.
Naye Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Handeni, Carlos, alibainisha kuwa malipo yote ya fidia yatatolewa moja kwa moja kupitia akaunti binafsi za wanufaika, jambo linaloimarisha usalama wa fedha na kuondoa hofu ya upotevu.
Wananchi walionufaika na fidia hiyo waliishukuru serikali, wakieleza kuwa hatua hiyo imewapa matumaini mapya ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.






