Serikali yazindua Mpango wa Kitaifa Kuimarisha Haki na Usalama wa Wanawake

πŸ“Œ Asema Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa wanapata haki na heshima wnayostahili

πŸ“ŒAzindua Mpango kazi wa Kitaifa wa Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama

πŸ“Œ Unalenga kushirikisha wanawake kikamilifu katika masuala ya Amani na Usalama

πŸ“Œ Ataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutokomeza dalili zinazoweza kuleta uvunjifu wa amani na usalama katika jamii

πŸ“Œ Asema kuzinduliwa kwa mpango kazi wa Amani na Usalama kunaonesha jinsi Tanzania inavyoheshimu na kutekeleza makubaliano ya kimataifa

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema wanawake ni chanzo kikuu cha msukumo wa maendeleo katika jamii, hivyo Serikali itaendelea kuhakikisha kila mwanamke nchini, awe mama au mtoto wa kike, anapata haki na heshima anayostahili.

Amesema wakati Serikali ikiendelea kuhakikisha wanawake wanapata haki zao ikiwemo usalama na amani, anatoa wito kwao kuendelea kujitambua na kuchangamkia kila aina ya fursa zinazojitokeza nchini.

Dk. Biteko aliyasema hayo wakati akizindua Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama 2025 – 2029, ikiwa ni utekelezaji wa Azimio Namba 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalohusu Wanawake, Amani na Usalama.

Azimio hilo, ambalo limeridhiwa na nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa ikiwemo Tanzania, linasisitiza na kutoa kipaumbele kwa ushiriki kamili wa wanawake katika hatua zote za ujenzi wa amani, uzuiaji na utatuzi wa migogoro, mazungumzo ya amani, ulinzi wa amani na ujenzi wa jamii baada ya migogoro.

Dk. Biteko alibainisha kuwa utekelezaji wa Azimio hilo unaonesha Tanzania siyo nchi ya kuridhia tu mipango ya kimataifa, bali inaheshimu makubaliano na maazimio hayo. Hali hiyo, alisema, inaimarisha hadhi ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, na kuifanya nchi kuwa mfano wa kuigwa kimataifa.

Akizungumzia utekelezaji wa Ajenda hiyo nchini, alisema Tanzania imepiga hatua kubwa na inaendelea vizuri. Kwa mujibu wa Gender Inequality Index 2021, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilishika nafasi ya 146 kati ya nchi 191 kutokana na maendeleo yaliyopatikana tangu miaka ya 1990 katika kuhimiza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake, kuboresha afya ya mama na mtoto pamoja na uwepo wa uwakilishi wa wanawake bungeni.

Aidha, kwa mujibu wa Global Peace Index 2021, Tanzania ilishika nafasi ya 58 kati ya nchi 163 zenye hali bora ya amani duniani.

Dk. Biteko aliongeza kuwa Tanzania imeendelea kuwapa wanawake nafasi katika maamuzi ya juu. Hadi Mei 2023, uwakilishi wa wanawake katika mfumo wa mahakama ulikuwa asilimia 46.6. Aidha, asilimia 22 ya askari polisi ni wanawake, asilimia 30 ya maafisa uhamiaji ni wanawake, na kati ya 785 wa mawakili wa serikali Tanzania Bara, wanawake ni 410 sawa na asilimia 52. Vilevile, Zanzibar ina jumla ya 76 wa mawakili wa serikali, ambapo wanawake ni 34 sawa na asilimia 44.

Pamoja na mafanikio hayo, alionya kuwa bado yapo masuala yanayohitaji msukumo zaidi. Kwa mujibu wa takwimu, asilimia 48.3 ya wanawake nchini wamewahi kufanyiwa ukatili. Mwaka 2015, asilimia 65 ya wanawake waliogombea nafasi za uongozi walikumbana na changamoto mbalimbali, ikiwemo matusi, huku asilimia 17 wakishambuliwa na asilimia 13 wakiombwa rushwa ya ngono.

Alisisitiza kuwa hali hiyo inaonesha bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuinua haki za wanawake. Mpango uliozinduliwa unalenga kuhakikisha matendo yasiyo ya haki yanatoweka na hadhi ya mwanamke inapanda zaidi.

Aidha, aliwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa nguvu kubwa ikiwemo kutoa elimu na kutokomeza dalili za uvunjifu wa amani na usalama, kama vile mila na desturi zenye madhara, wahamiaji haramu, unyanyasaji wa kijinsia na matumizi ya dawa za kulevya.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, alitaja baadhi ya vipaumbele vya Mpango huo kuwa ni uzuiaji wa migogoro, ushiriki wa wanawake katika kufanya maamuzi kwenye ngazi zote, mikataba ya amani, pamoja na ulinzi wa wanawake na wasichana dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia wakati na baada ya migogoro.

Alisema mpango huo utaleta matokeo chanya katika amani na usalama wa wanawake, na kuwezesha Serikali kutimiza wajibu wake kitaifa, kikanda na kimataifa katika kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu kwenye masuala hayo.

Naye, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax, alisema uzinduzi wa mpango huo ni tukio la kihistoria na lenye uzito mkubwa si kwa taifa pekee bali pia kimataifa katika kujenga dunia yenye haki, usawa na amani.

Aliongeza kuwa ni kielelezo cha dhamira ya Serikali katika kushirikisha wanawake kwenye masuala ya amani, usalama na uongozi. Pia alimshukuru Rais Samia kwa kuwa sauti ya kimataifa inayosisitiza dunia yenye haki na amani. Tanzania, alisema, imetambulika duniani kwa mchango mkubwa katika misheni za kulinda amani, ambapo hadi sasa imetuma takribani askari 1,500, wakiwemo wanaume na wanawake.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Zanzibar, Riziki Pembe, alisema mpango huo ni muhimu kwa maendeleo ya wanawake na taifa kwa ujumla, kwani maendeleo huzaliwa pale ambapo kuna amani na usalama.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tayari inatekeleza ajenda hiyo kwa vitendo. Alitoa mfano wa ongezeko la nafasi za uongozi kwa wanawake, ikiwemo uteuzi wa majaji wanawake wasiopungua sita, tofauti na ilivyokuwa awali. Pia, Serikali inazingatia bajeti zinazojumuisha masuala ya kijinsia katika wizara zote.

Naye, Anna Mutavati, Mkurugenzi wa UN-Women katika Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, aliipongeza Tanzania kwa kuzindua ajenda hiyo na kusisitiza kuwa bado inaendelea kuwa mfano wa kuigwa katika masuala ya amani na usalama, ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *