📌Mkoa wa Mwanza wapokea Bil 66.7 kupeleka Umeme Vitongojini
📌 Kaya 19,878 kunufaika na umeme wa REA Vitongojini
📌 Vitongoji 619 kufikiwa na Umeme Mkoani Mwanza.
📌Wakandarasi wasisitizwa kujiepusha na Vitendo vya Rushwa
📍MWANZA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia Sh. bilioni 66.7 kupeleka umeme katika Vitongoji 619 ambapo Kaya 19,878 zitafikiwa na Huduma hio ya Umeme wa REA.
Hayo yamesemwa jana Jijini Mwanza na Mkuu wa mkoa huo Said Mtanda, wakati wa kikao cha kumtambulisha mkandarasi TIBEA Company Limited pamoja na White City International Contractors ambao wamepewa dhamana ya kusambaza huduma hio katika Vitongoji 619 vya Mkoa huo kwa kipindi cha Miaka Mitatu.
Mtanda amesisitiza Mradi huu ni Mkubwa hivyo Matumaini yake kwa Wananchi wa Ukerewe,Misungwi,Magu,Sengerema na Kwimba wanakwenda kunufaika na Mradi huu hivyo amewataka wakandarasi waliopewa kazi hio kufanya kazi kwa weledi na kuepuka Vitendo vya Rushwa wakati wa kuwaunganishia Wananchi Umeme kitendo ambacho sio kizuri kwani kinaharibu taswira ya Kampuni yao na endapo itabainika Sheria itachukua Mkondo wake ikiwemo kutokupewa kazi nyingine yoyote.




“Ni Vizuri mkafanya kazi kwa Uadilifu, Mkaepuke Rukwa wakati wa kuwaunganishia Umeme Wananchi, amesisitiza Mtanda”.
Aidha, Mtanda ameomba Wananchi watakaofikishiwa huduma hio ya Umeme kuwapokea Vizuri Wakandarasi, Amesisitiza ni muhimu Wakandarasi hao kushirikisha ngazi zote za Serikali mpaka kwa Walengwa Wananchi kwani itarahishisha kazi, Pia ametaka Wananchi waelezwe sifa za Mradi, utaratibu wa kuweka umeme kwenye Nyumba zao upoje ili kuepuka usumbufu na Mazingira ya Uwepo wa Rushwa hivyo ni muhimu kuwaelimisha Wananchi nia ya Serikali ni kuwahudumia wote.
Kwa upande wake, Mhandisi, Seif Abduli, Mhandisi wa Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) amesema TIBEA Company Limited atahudumia Vitongoji 313 kwa Wilaya ya Sengerema na Kwimba huku gharama yake ikiwa Bil. 33.7, Kwa upande wa White City International Contractors atahudumia Vitongoji 306 Wilaya ya Ukerewe,Misungwi pamoja na Magu ambapo gharama yake ni Bil 32.7.
Mhandisi Seif amesisitiza Mradi huu ni Mkubwa na wakimkakati lengo likiwa Watanzania wanapata Umeme hivyo Serikali imeweka jitihada kubwa ambapo imeleta kifaa Maalum kinachoitwa OMETA ambapo kitawasaidia wananchi waishio Vijijini wasio na uwezo wa Kufanya Wiring kuunganishiwa umeme kupitia kifaa ili asitokee Mwananchi atakaye achwa nyuma na Huduma ya Umeme Vitongojini.








