Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), Bakari Shime, amesema licha ya ushindi walioupata dhidi ya Ethiopia, mechi hiyo ilikuwa ya ushindani mkali na yenye presha kubwa.
Twiga Stars ilipata ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa raundi ya pili ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON 2026), uliochezwa jijini Dar es Salaam.
Mchezo wa marudiano unatarajiwa kuchezwa Oktoba 28 katika mji wa Bahir Dar, Ethiopia.
Shime alisema kikosi chake kilimiliki mchezo kipindi cha kwanza lakini kilikosa kasi ya kumalizia nafasi nyingi za wazi.
“Wachezaji walicheza vizuri, lakini tulikosa ufanisi mbele ya lango. Tulihitaji ushindi mkubwa zaidi ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu,” alisema Shime.
Aliongeza kuwa Ethiopia walionesha nidhamu ya hali ya juu na kuufanya mchezo kuwa mgumu zaidi.
“Ilikuwa mechi ya moto, tulikutana na wapinzani wanaojua mfumo wetu. Nawapongeza wachezaji wangu kwa uthubutu na umakini waliouonesha,” alisema.
Nahodha wa timu, Opa Clement, alisema ushindi huo ni muhimu kwao kabla ya mchezo wa marudiano.
“Tunashukuru kwa ushindi huu, tunajua bado kazi haijaisha. Tunarejea mazoezini kuangalia makosa yetu kabla ya kwenda Bahir Dar,” alisema Opa.
Katika michezo mingine ya raundi hiyo, Zambia ikiwa ugenini iliifunga Namibia 4-2, huku DR Congo ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya mabingwa watetezi Afrika Kusini.




