Msimu wa 2020/2021, ambao hadi sasa unabaki kuwa msimu wa mwisho Klabu ya Simba SC kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliandikwa kwa historia kubwa kutokana na uimara wa kikosi, ushindani wa hali ya juu na mchango mkubwa wa wachezaji wake muhimu.
Katika msimu huo, wanaume watatu walichangia jumla ya magoli 58, wakionesha ubora na mshikamano mkubwa wa kikosi. Medie Kagere alifunga magoli 13 na kutoa pasi tatu za mabao, Luis Miquissone akifunga magoli tisa na kutoa pasi 10 za mabao, huku Clatous Chama akifunga magoli nane na kutoa pasi 15 za mabao.
Msimu huo pia ulitawaliwa na tuzo mbalimbali, ambapo John Bocco alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi (MVP), Clatous Chama akatwaa tuzo ya Kiungo Bora, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ akashinda tuzo ya Beki Bora, huku Aishi Manula akinyakua tuzo ya Golikipa Bora.
Katika safu ya ushambuliaji, Simba ilikuwa na nguvu kubwa ikiongozwa na Mugalu, Medie Kagere na John Bocco, wakati safu ya kiungo ikijaa vipaji na wapambanaji kama Bwalya, Morrison, Kahata, Fraga Vieira, Mkude, Ndemla, Chama, Luis Miquissone, Mzamiru, Kichuya na Dilunga.
Simba ya msimu huo haikuwa tu na wachezaji wenye majina makubwa, bali pia ilikuwa na kikosi cha wapambanaji wa kweli, wachezaji waliokuwa tayari “kuvuja jasho” kwa ajili ya nembo ya klabu. Hilo linadhihirika wazi katika orodha ya wafungaji bora wa ligi msimu huo, ambapo John Bocco alikuwa kinara kwa magoli 16, akifuatiwa na Mugalu aliyefunga magoli 15 na Kagere aliyefunga magoli 13.
Kwa upande wa uongozi, Simba iliongozwa na Mzee Mohammed Dewji (MO) akiwa Mwenyekiti wa Bodi, Barbara Gonzalez akiwa Mtendaji Mkuu (CEO), huku marehemu Hans Pope akiwa bado hai na mchango wake ukiwa sehemu ya mafanikio ya klabu katika kipindi hicho.
Msimu wa 2020/2021 unabaki kuwa kumbukumbu muhimu kwa mashabiki wa Simba SC kama mfano wa kikosi kilichojengwa kwa ubora, mshikamano na mapambano ya dhati ndani ya uwanja.




