Mwanariadha wa kimataifa kutoka Tanzania, Alphonce Felix Simbu, ameweka historia kubwa baada ya kushinda medali ya dhahabu katika mashindano ya riadha ya dunia yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa wa Japan, jijini Tokyo.
Simbu, mwenye umri wa miaka 33, alimaliza mbio za marathon kwa muda wa saa 2:09:48, akimshinda mpinzani wake Amanol Petros wa Ujerumani kwa tofauti ya sekunde 0.03 pekee, ambayo ni rekodi ya tofauti ndogo zaidi kwenye historia ya mashindano ya marathon duniani.
“Nimeweka historia leo, ikiwa ni medali ya kwanza ya dhahabu ya Tanzania katika mashindano ya dunia,” alisema Simbu mara baada ya kukamilisha mbio hizo kwa kishindo.
Mwanariadha huyo aliongeza kuwa ushindi huo ni matokeo ya subira na moyo wa kutokata tamaa: “Nakumbuka mwaka 2017 kwenye mashindano ya dunia jijini London nilishinda medali ya shaba. Baada ya hapo nilishiriki mara nyingi lakini sikuweza kushinda tena medali yoyote. Hatimaye leo ndoto yangu imetimia, nilijiambia sitakata tamaa.”
Ushindi wa Simbu si tu umempa heshima binafsi, bali pia umeiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia katika mbio ndefu, ukionesha maendeleo makubwa ya riadha nchini.










