Wachezaji sita wa Taifa Stars wameweka historia kwenye mchezo wa ufunguzi wa fainali za CHAN 2025, baada ya Tanzania kuibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Burkina Faso katika mashindano yanayoendelea Kenya na Uganda.

Abdul Suleiman ‘Sopu’ alifunga bao la kwanza la mashindano kwa penalti, akiwa pia mchezaji wa kwanza kufunga kwa mkwaju huo katika CHAN ya mwaka huu. Bao hilo pia limekuwa la kwanza kufungwa kipindi cha kwanza tangu mwaka 2016, Rwanda.
Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alifunga bao la pili kwa kichwa dakika ya 71, na kuweka rekodi ya kuwa mfungaji wa kwanza wa bao lisilotokana na penalti katika fainali hizi.
Idd Selemani ‘Nado’ ndiye aliyetoa pasi ya bao hilo, hivyo kuingia kwenye kumbukumbu kama mchezaji wa kwanza kutoa asisti mwaka huu.
Kipa Yacoub Suleman ameweka rekodi ya kwanza ya clean sheet, huku Feisal Salum ‘Fei Toto’ akitwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi.
Mudathir Yahaya yeye amekuwa wa kwanza kuonyeshwa kadi ya njano kwenye mashindano haya.