Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Zungu, amewapongeza wahitimu wa Programu ya Mwanamke Kiongozi kwa juhudi zao na mchango wao katika kuimarisha nafasi za wanawake katika uongozi wa jamii na taasisi.
Akihutubia katika Mkutano wa 8 wa Uongozi pamoja na Mahafali ya 11 ya Programu ya Mwanamke Kiongozi (Female Future), yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City leo, Zungu amesema kuwa programu hiyo imekuwa chocheo cha maendeleo ya wanawake, ikiwafikia zaidi ya wanawake 600 na makampuni 180 tangu ilipozinduliwa mwaka 2016. Programu hii, alisema, imechangia kuongeza nidhamu, uwajibikaji na uwezo wa wanawake kushika nafasi za uongozi katika sekta mbalimbali.
Spika Zungu pia amewashukuru wadau, mashirika ya fedha, sekta binafsi na serikali kwa michango yao katika matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo, akibainisha kuwa kila mwaka watoto elfu 10 wanazaliwa na matatizo ya moyo, huku elfu 4 wakiihitaji upasuaji. Aliwapa wito wadau kuendelea kuchangia katika matibabu, vifaa na kampeni za uchunguzi mapema, akisisitiza kuwa kinga ni bora kuliko tiba.




Aidha, Zungu amewapongeza wahitimu na kuwataka kuendelea kuwa viongozi wema, wajasiriamali na mashirika ya kijamii, akibainisha kuwa mafanikio haya yataendelea kukua ikiwa tutashirikiana na kushikamana.
Spika Zungu ameweka wazi kuwa Bunge la Tanzania litaendelea kuwa mdau wa kwanza kuhakikisha mazingira ya kisheria na kijamii yanawezesha maendeleo ya wanawake, na kwamba usawa wa kijinsia ni sehemu muhimu ya maendeleo ya taifa.
“Tumeshiriki katika safari ya miaka mingi ya maendeleo, na ninawahakikishia kuwa Bunge litaendelea kusimamia usawa, haki, na maendeleo ya wanawake nchini,” amesisitiza.
Wanawake viongozi waendelea Kung’ara


Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba-Doran, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii, taasisi na taifa kwa ujumla.
Akitoa salamu za utangulizi katika mkutano huo Ndomba-Doran amesema mkutano huo umeendelea kuwa jukwaa muhimu la kujenga uwezo, kubadilishana uzoefu na kuhamasisha kizazi kipya cha wanawake viongozi.
Ameeleza kuwa maadhimisho hayo yamebeba ujumbe wa Siku ya Wanawake Duniani wa mwaka huu unaosema “Haki, Usawa na Hatua kwa Wanawake na Wasichana Wote,” ukiwa ni wito wa pamoja kwa jamii kuendeleza haki, kuimarisha usawa na kuchukua hatua madhubuti kwa manufaa ya kila mwanamke na msichana.
Ndomba-Doran ameeleza kuwa wahitimu wa Cohort ya 11 wanatarajiwa kuendeleza mshikamano na kuwainua wanawake wengine ili kufungua fursa zaidi na kufanikisha ndoto za wengi. Alibainisha kuwa mwaka huu programu ya Female Future imetoa wahitimu 158, idadi kubwa zaidi tangu kuanzishwa kwake, jambo linaloashiria kukua na kuimarika kwa mpango huo.
Tangu kuanzishwa kwake, programu ya Female Future imeendelea kuwa chachu ya mabadiliko kwa kuwajengea wanawake uwezo katika maeneo ya uongozi, uelewa wa bodi za wakurugenzi, mawasiliano ya kimkakati na ujasiri wa kushika nafasi za juu za maamuzi. Kupitia mafunzo, ushauri elekezi (mentorship) na mtandao wa kitaalamu, wanawake wengi wamefanikiwa kupandishwa vyeo, kuchaguliwa katika bodi za taasisi mbalimbali na kushika nyadhifa muhimu katika sekta binafsi na za umma.



Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Rahma Kisuo, amewataka waajiri kuzingatia haki, usawa na staha mahali pa kazi. Aliwashukuru wadhamini na waajiri wanaoendelea kuwekeza katika mafunzo na maendeleo ya wanawake, akibainisha kuwa hata baadhi ya wabunge wanawake wamenufaika na programu hiyo.
Ameeleza kuwa uwepo wa Rais Samia Suluhu Hassan, ni mfano hai na chanzo kikubwa cha hamasa kwa wanawake nchini kuthubutu, kujiamini na kuchukua nafasi zao za uongozi kwa ujasiri na weledi.
Aidha, wahitimu wa programu hiyo wamepongezwa kwa moyo wao wa kujitolea kwa jamii, baada ya kuchangia shilingi milioni 35 kusaidia watoto wenye matatizo ya moyo wanaopatiwa matibabu katika Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI). Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni ushahidi kuwa mafunzo wanayoyapata yanatafsirika katika vitendo vinavyogusa maisha ya watu.
Imeelezwa pia kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia inachangia asilimia 70 ya gharama za matibabu ya watoto hao, huku juhudi za wadau zikiongeza nguvu katika kuokoa maisha na kujenga jamii yenye huruma.
Kwa ujumla, Programu ya Female Future imeendelea kuthibitisha kuwa kuwekeza katika uongozi wa wanawake ni kuwekeza katika maendeleo endelevu ya taifa. Hata hivyo, viongozi walisisitiza umuhimu wa wanawake kuendelea kudumisha upendo, mshikamano na ushirikiano ili kufikia mafanikio makubwa zaidi katika safari ya kujenga taifa lenye usawa na fursa kwa wote.




