Thursday, March 12, 2026
spot_img
HomeElimuTaasisi ya Nelson Mandela na Global education Link wakubaliana kuimarisha tafiti na...

Taasisi ya Nelson Mandela na Global education Link wakubaliana kuimarisha tafiti na ubunifu


Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kwa kushirikiana na Taasisi ya Global Education Link Ltd wamesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano yenye lengo la kukuza tafiti, ubunifu na maendeleo ya kisayansi.

Makubaliano hayo  yatakayosaidia kuandaa kizazi kipya kitakacholeta mapinduzi ya kiuchumi na kiteknolojia Barani Afrika na duniani kwa ujumla. 

Ushirikiano huo unatarajiwa kufungua milango ya fursa mpya katika sekta ya elimu, utafiti na ubunifu, pamoja na kuitangaza taasisi hiyo kimataifa ili dunia itambue kuwa Tanzania ina taasisi inayozalisha vipaji na teknolojia za kisasa kupitia ushirikiano na vyuo vikuu mbalimbali vya nje ya nchi.

Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Makamu Mkuu wa Taasisi ya Nelson Mandela, Profesa Maulilio Kipanyula, alisema Afrika ina hazina kubwa ya vipaji ambavyo vikisimamiwa na kupangwa vizuri vinaweza kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.

Profesa Kipanyula alisisitiza kuwa ubunifu na maendeleo ya kisayansi hayawezi kufikiwa bila ushirikiano wa taasisi mbalimbali, akibainisha kuwa makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kuongeza idadi ya wanafunzi, hususan wanafunzi wa kimataifa, pamoja na kuchangia kukuza uchumi.

Alisema makubaliano hayo ni ya kimkakati katika kuhakikisha elimu inayotolewa inaendelea kuimarika kimataifa kwa kuvutia vipaji vya vijana kusoma na kuwasilisha bunifu zao kupitia Taasisi ya Nelson Mandela. 

Aidha, alieleza kuwa anatamani kuona taasisi hiyo ikiendelea kuzalisha na kulea vipaji vya vijana pamoja na ubunifu mbalimbali utakaosaidia kuchochea maendeleo katika majukwaa ya kitaifa na kimataifa. 

“Tunataka tafiti zetu na matokeo yake yawafikie wananchi kwa haraka zaidi, ambapo ubunifu na maarifa vitakuwa na mchango mkubwa kwa jamii. Utafiti na ubunifu lazima viwe na uwezo wa kutatua changamoto za watu,” alisema Profesa Kipanyula.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Global Education Link Ltd, Abdullmalik Mollel, alisema ushirikiano huo umejikita katika kuimarisha masuala ya kitaaluma, uwekezaji na matumizi ya teknolojia ili kuongeza tija katika sekta ya elimu na uchumi.

Alisema elimu inayotolewa kwa wanafunzi inapaswa kuwa na mchango wa moja kwa moja katika kukuza uchumi na maendeleo kwa kutumia teknolojia, maarifa na mitaji. 

“Elimu anayopewa mwanafunzi inapaswa kusaidia kukuza uchumi na kuleta maendeleo kupitia teknolojia, maarifa na uwekezaji. Ushirikiano wa maarifa kati ya vyuo vikuu mbalimbali utaongeza tija katika kukuza uchumi unaotegemea teknolojia,” alisema Mollel.

Aliongeza kuwa makubaliano hayo ni mwanzo wa safari ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya taasisi hizo mbili, wenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa vyuo vikuu na kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya elimu, utafiti na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments