Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaendelea kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, kupitia ujenzi wa miundombinu ya barabara na masoko.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga, Nassir Kilusha, amesema kuwa kiasi cha shilingi bilioni 20.361 kimepokelewa kupitia mradi huo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo:
- Ujenzi wa jengo la ofisi za usimamizi wa mradi,
- Ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 13.3,
- Ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua,
- Uwekaji wa taa za barabarani.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo umefikia zaidi ya asilimia 80.
Manufaa kwa Wananchi
Bw. Kilusha amesema kabla ya mradi huo, barabara zilikuwa na changamoto za vumbi, mashimo, matope na maji kujaa kwenye makazi ya watu, hali iliyosababisha usumbufu kwa wananchi. Hata hivyo, hali imebadilika baada ya maboresho yaliyofanywa kupitia TACTIC.
“Sasa maji hayatuami kutokana na mitaro, biashara zinaendelea hadi usiku kwa sababu ya taa, usalama umeimarika, uwekezaji umeongezeka, thamani ya viwanja na nyumba imepanda, na shughuli za usafiri na usafirishaji zimeongezeka,” alisema Kilusha.




Aidha, ameongeza kuwa kwa sasa Halmashauri inaendelea na ujenzi wa Soko Kuu la mazao ya nafaka katika eneo la Kanondo kwa gharama ya shilingi bilioni 7.4. Soko hilo litakuwa na miundombinu ya kisasa ikiwemo maegesho ya magari, maeneo ya mawakala, maghala ya kuhifadhia mazao na sehemu ya huduma za chakula. Ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Desemba 2025.
Mapato ya Halmashauri Kuongezeka
Kuhusu mapato, Bw. Kilusha amesema mwaka wa fedha uliopita Halmashauri ilikusanya shilingi bilioni 3.4, huku mwaka huu ikitarajia kukusanya bilioni 3.9, sawa na ongezeko la shilingi milioni 500. Ameitaka jamii kushirikiana na Serikali kulinda miundombinu iliyojengwa ili idumu kwa muda mrefu.
Kauli za Wadau
Kwa upande wake, Mratibu wa TACTIC kutoka TARURA Sumbawanga, Mhandisi Emmanuel Kudema, amesema kabla ya mradi walikuwa na kilomita 32.89 za barabara za lami pekee, lakini sasa zimeongezeka kwa kilomita 13.03 na kufikia jumla ya kilomita 45.92. Hali hiyo imepunguza gharama za matengenezo na kuboresha mtandao wa barabara.




Wananchi nao wameshukuru Serikali kwa mradi huo:
- Nasma Kazumari, mkazi wa Kata ya Katandala, amesema barabara mpya na taa za barabarani zimeboresha biashara zao na mazingira ya mji yamekuwa safi na salama.
- Baraka Edwin, dereva bajaji kutoka Kata ya Mafulala, amesema barabara nzuri zimewapunguzia muda wa safari na kuongeza idadi ya abiria. Ameomba wananchi wenzake wasitupe taka kwenye mitaro ili kuzuia kuziba na kuharibu miundombinu.
- Getricia Bomani, aliyeajiriwa katika ujenzi wa Soko la Kanondo, amesema mradi huo umemsaidia kiuchumi na unatarajiwa kuongeza thamani ya mazao, hata kufungua masoko ya kibiashara hadi nchi jirani za Congo na Zambia.








