TALIRI yajipanga kushirikiana na wafugaji kuboresha Sekta ya Mifugo kwa teknolojia bunifu

Dar es Salaam — Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Prof. Erick Komba, amesema taasisi hiyo iko tayari kushirikiana kwa karibu na wafugaji pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya mifugo nchini, ili kubaini na kutatua changamoto zinazowakabili wafugaji kwa kutumia teknolojia bora zinazolenga kuongeza tija katika uzalishaji.

Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwl. Julius K. Nyerere, jijini Dar es Salaam, Prof. Komba alisema ushirikiano kati ya taasisi na wadau unalenga kuongeza mchango wa sekta ya mifugo katika pato la Taifa.

“Katika kipindi hiki cha Sabasaba, tupo hapa kwa ajili ya kutoa elimu na kusambaza teknolojia zetu kwa wafugaji, ikiwemo teknolojia ya malisho, mbegu za malisho, vyakula vya mifugo, na mbari bora za mifugo,” alieleza Prof. Komba.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TALIRI Kanda ya Mashariki, Dkt. Zabron Nziku, alisema kuwa ili mfugaji aweze kufanikisha uzalishaji bora, ni lazima awe na malisho ya kutosha pamoja na aina bora ya mifugo inayofaa kwa mazingira ya Tanzania.

“Tumeleta teknolojia ya boksi la kufungia majani ili yaweze kuhifadhiwa vizuri kwa matumizi ya baadaye, hasa katika vipindi vya kiangazi ambapo upatikanaji wa majani unakuwa mgumu,” alisema Dkt. Nziku.

Alifafanua kuwa boksi hilo ni rahisi kutumia na linamwezesha mfugaji wa hali yoyote kutengeneza marobota ya majani (hay) kwa gharama nafuu. “Watu wawili wanaweza kutengeneza marobota 350 kwa mwezi, na robota moja linaweza kulisha ng’ombe wawili kwa siku,” aliongeza.

Naye, Meneja wa Sehemu ya Uhaulishaji wa Teknolojia, Bw. Gilbert Msuta, aliwahimiza wafugaji na wadau mbalimbali wa sekta ya mifugo kutembelea banda la TALIRI katika maonesho hayo ili kujipatia elimu ya ufugaji bora na teknolojia zinazoweza kuongeza uzalishaji na kipato.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *