TALIRI yashinda tuzo Nanenane 2025 kwa teknolojia za kuku Horasi na malisho bora

Kwa mara ya pili mfululizo, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) imeibuka mshindi wa kwanza katika kundi la Taasisi za Umma zinazotoa Mafunzo na Utafiti kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ‘Nanenane’ yanayofanyika katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Tuzo hiyo imekabidhiwa na Rais Samia Suluhu Hassan tarehe 08/08/2025.

Akizungumzia tuzo hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI Prof. Erick Vitus Komba amesema kuwa teknolojia bora za mifugo zilizofanyiwa utafiti na TALIRI zimechangia ushindi wa upatikanaji wa tuzo hiyo.

“Tulikuwa na teknolojia ya kuku wa asili aina ya Horasi ni miongoni mwa teknolojia tulizomuonesha Mhe. Rais ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya sikukuu ya wakulima duniani ‘Nanenane’ amesema Prof. Komba.

Prof. Komba ameeleza kuwa teknolojia hiyo inazalishwa na kufanyiwa uchaguzi wa kuku aina ya horasi ili kupata kizazi kilichoboreshwa ambacho kitakuwa na uzalishaji mkubwa zaidi kuliko kuku wengine wa asili.

Aidha, Prof. Komba ameeleza kuwa teknolojia zingine zilizopelekea ushindi huo ni teknolojia ya utafiti wa malisho na kufanikiwa kusajili mbegu tano za malisho pamoja teknolojia za uzalishaji wa malisho yaliyovundikwa ambayo ni marobota na majani vunde, teknolojia za mbari bora za mifugo pamoja na vyakula vya mifugo.

“Shukrani za dhati kwa Rais wetu Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa tuzo hii TALIRI itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa kushirikiana na wafugaji na wadau mbalimbali wa mifugo ili kuwezesha ufugaji wenye tija nchini” amesema Prof. Komba.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *