πππΆππΎπΆ ππΆ ππΆππΆππΎ ππΆ πΏπΎπΏπΎ ππΆ πππππ½πΆ ππΆπΏπΎππππππΆ ππππ½πΎππΎππΎ ππΆππΆππ·πππΎ ππΆ π°ππΎππΉπππΎ π½ππ.
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limezindua rasmi kampeni ya “Shangwe la Sikukuu na TANAPA” leo, Desemba 13, 2024, jijini Arusha. Kampeni hii inalenga kuhamasisha Watanzania na wageni kutoka mataifa mbalimbali kutembelea Hifadhi za Taifa katika msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya 2025.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayeshughulikia Maendeleo ya Biashara TANAPA, Jully Bede Lyimo, alisema TANAPA inajivunia kuwa na hifadhi za taifa 21 ambazo ni miongoni mwa bora barani Afrika na duniani.
“Hifadhi hizi zipo karibu kila mkoa wa Tanzania. Ushiriki wa Watanzania katika kuzitembelea siyo tu unawapatia furaha ya kufurahia uasili wa nchi yetu, bali pia unasaidia kutangaza vivutio vyetu,” alisema Kamishna Lyimo.
Aliongeza kuwa mapato yanayotokana na viingilio vya hifadhi hizi huchangia pato la taifa, ambalo hutumika kuboresha huduma za msingi kama ujenzi wa barabara, viwanja vya ndege, hospitali, na shule.




Kwa zaidi ya miongo sita tangu kuanzishwa kwake, TANAPA imeendesha kampeni mbalimbali kuhamasisha Watanzania kutembelea vivutio vya utalii vinavyopatikana ndani ya hifadhi hizo.
Kwa mwaka huu, kampeni ya “Shangwe la Sikukuu na TANAPA” inalenga kufikia Watanzania kwa njia ya ofisi kwa ofisi, mtaa kwa mtaa, na mlango kwa mlango ili kuwahamasisha kutembelea Hifadhi za Taifa.









