Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), limewataarifu wateja wake kuwa kutakuwa na maboresho ya mfumo wa manunuzi ya umeme wa LUKU yatakayofanyika kesho Jumatano usiku kuamkia Alhamisi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maboresho hayo yatafanyika kuanzia saa 6:00 usiku hadi saa 8:00 usiku, sawa na muda wa saa mbili.
Kutokana na maboresho hayo ya mfumo, huduma ya kununua umeme kupitia mfumo wa LUKU haitapatikana kwa muda huo.
Hivyo, TANESCO imewashauri wateja wake kununua umeme mapema kabla ya muda wa maboresho ili kuepuka usumbufu wowote unaoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa kazi hiyo ya kiufundi.





