Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri, Profesa John Safari, amesema kumekuwa na mabadiliko chanya katika ushiriki wa vyama vya kijamii na vya ushirika vinavyolenga kuchangia upatikanaji wa haki ya chakula kwa wanawake, wanaume, vijana na watoto nchini Tanzania, Kenya na Uganda ifikapo mwaka 2027.

Akizungumza mwishoni mwa wiki na wadau kutoka vyama vya kijamii na vya ushirika 21, Prof. Safari alisema dhamira hiyo inalenga kuimarisha mifumo ya chakula yenye usawa na endelevu katika jamii.
Wadau hao walikuwa wakipatiwa mafunzo ya uongozi wa mabadiliko (Leadership for Change – LCF) kupitia Mradi wa miaka mitano wa Kuimarisha Uwezo wa Vyama vya Ushirika na Asasi za Kiraia (CACOSMBO). Mradi huo unatekelezwa na MoCU kwa ufadhili wa Shirika la We Effect Afrika Mashariki.
“Miongoni mwa matokeo yanayotarajiwa kupitia mradi huu ni kujenga mashirika yenye nguvu, kuboresha maisha ya wanajamii, kuimarisha uwezo wa kukabiliana na changamoto, kuongeza upatikanaji wa haki na usawa, kusisitiza makazi bora, kuendeleza usawa wa kijinsia, pamoja na kukuza mfumo wa chakula ulio sawa na endelevu,” alisema Prof. Safari.
Kwa upande wake, Meneja Msaidizi wa Mradi huo, Ernest Hizza, alisema mpango huo umejikita katika kujenga uwezo wa viongozi na wasimamizi wa vyama vya kijamii na vya ushirika ili waweze kuleta mageuzi ya kweli.
“Tulibaini changamoto kubwa ipo kwenye uongozi usio imara unaosababisha taasisi nyingi kushindwa kusimama. Hivyo, tukaona umuhimu wa kuanzisha programu hii ya kuwafundisha uongozi wa mabadiliko, uongozi wa kuona mbali, ili vyama hivi viwe na tija na viweze kusimama kwa uimara,” alieleza Hizza.

na vyama vya kijamii, kwa kuvijengea uwezo ili kuleta tija na mabadiliko chanya ya uendeshaji wa taasisi hizo.


