Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta ya ulinzi na viwanda baada ya Kituo cha Teknolojia ya Magari na Mitambo Tanzania (TATC Nyumbu) kusaini hati ya mashirikiano ya kihistoria na Kampuni ya STREIT Group kutoka Falme za Kiarabu (UAE).
Mkataba huu unalenga kuanzisha uzalishaji wa magari ya kijeshi nchini, hatua itakayoimarisha ulinzi na kufungua fursa mpya za kiteknolojia kwa Taifa.
Akizungumza Septemba 29, 2025, baada ya kusainiwa kwa mkataba huo na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda hicho, Waziri wa Ulinzi na JKT, Dk. Stergomena Lawrence Tax, amesisitiza umuhimu wa TATC Nyumbu kutumia fursa hiyo.




Pamoja na uzalishaji, tutaweza kupata teknolojia mpya ambayo hatukuwa nayo awali. Nasisitiza TATC Nyumbu itumie fursa hii kikamilifu,” Dkt. Tax alielekeza.
Aidha, Waziri Tax ameielekeza STREIT Group kukamilisha ujenzi wa jengo la kiwanda ndani ya muda uliopangwa wa miezi 12 ili kazi ya uzalishaji iweze kuanza mara moja.
Akizungumzia uwekezaji huo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) Jenerali Jacob Mkunda ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji. Alibainisha kuwa mazingira haya yanachochea wadau mbalimbali kuja nchini kuwekeza katika sekta mbalimbali.





Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TATC Nyumbu, Balozi mstaafu Luten Jenerali Wynjones Kisamba, amethibitisha kuwa tayari wamefanikiwa kukamilisha utafiti na sasa wanakwenda moja kwa moja kwenye hatua ya uzalishaji.
Naye Mwenyekiti wa STREIT Group, Guerman Goutorow, ameahidi mradi huo kukamilika ndani ya muda uliopangwa, akionyesha kujitolea kwao kutekeleza makubaliano hayo kwa wakati.




