Benki ya Biashara ya Tanzania (TCB) na Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT) wameingia makubaliano ya kuendeleza matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali kwa wanawake na vijana kupitia vikoba vinavyoendeshwa kijamii.

Ushirikiano huo unalenga kuongeza ujumuishwaji wa kifedha na kubuni majukwaa yatakayobadilisha maisha ya wananchi.
Hadi Julai 2025, zaidi ya vikoba 670,000 vimesajiliwa nchini, vikiwa na wanachama zaidi ya milioni saba na akiba inayozidi Sh trilioni 1.7. Takribani asilimia 50 ya wanachama hao ni wanawake, hali inayoonyesha mchango mkubwa wa mfumo huo katika kuchochea usawa wa kijinsia kwenye maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Dijitali wa TCB, Jesse Jackson, alisema mafanikio hayo ni ushahidi kuwa benki inaendelea kuwekeza kwenye teknolojia za kisasa ili kuwa kinara wa utoaji wa huduma bora na za kisasa nchini.




Alisema ushirikiano na FSDT utaimarisha uwekaji wa akiba kidijitali kwa kuongeza ukubwa wa data na uwezo wa vikundi kukopesheka. Pia utahusisha matumizi ya kliniki za mafunzo zinazotolewa na FSDT ili kubuni bidhaa mpya zenye thamani, hasa kwa wanawake na vijana.
Kwa mujibu wa Jackson, malengo ni kufanya kampeni kuanzia ngazi ya chini hadi kufikia vikundi vingi zaidi, na kusajili vikundi zaidi ya milioni moja kufikia Desemba 2026. Hatua hiyo inatarajiwa kuleta mchango mkubwa katika kupanua wigo wa huduma za kifedha nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa FSDT, Erick Massinda, alisema taasisi yake itaendelea kuunga mkono jitihada zinazoongeza upatikanaji wa huduma za kifedha za kidijitali ili kuboresha maisha ya wananchi, hususan makundi yaliyosahaulika kama wanawake na vijana. Alibainisha kuwa taarifa za mienendo ya kifedha ya wanachama zitatumika kubuni bidhaa kama mikopo yenye tija, uwekezaji na bima.



