TFF : Taifa Stars imefuzu CHAN

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema hata kama Timu ya Taifa (Taifa Stars itafungwa na Sudan, itashiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), kwa sababu ni wenyeji wa michuano hiyo.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Ndimbo, amebainisha hayo baada ya mashabiki kuonekana kutoelewa nafasi ya Stars endapo itapata matokeo mabaya huku baadhi wakiuliza kwa nini Tanzania inacheza michezo ya kufuzu wakati ni mmoja kati ya wenyeji wa fainali hizo.

Ndimbo alisema kanuni zinaruhusu wenyeji wa michuano na fainali kucheza michezo ya kufuzu ili kuwafanya wapande viwango kama wakishinda na kuwekwa kwenye ‘poti’ la juu ili kupata timu rahisi za kucheza nazo.

“Hata kama hatutapata matokeo mbele ya Sudan bado tutacheza fainali hizo kwa sababu kwa mujibu ya utaratibu wenyeji wote watatu, Tanzania, Kenya na Uganda wote watakuwemo.

Kuna njia mbili ya kucheza fainali hizo, kuna kufuzu kwa uenyeji na kufuzu kwa nguvu za uwanjani, kizuri ni hata kama ni mwenyeji wa fainali au michuano, ukifuzu kwa kushinda uwanjani utakuwa na wakati mzuri wa kuwepo kwenye poti ambalo linaweza kukurahisishia kupata kundi ambalo halitakupa tabu, lakini ukifuzu kwa uenyeji tu huna chaguo unaweza kuwekwa poti lolote lile, hapo sasa unaweza kukumbana na kundi gumu,” alisema Ndimbo.

Aliongeza wanauchukulia kwa umuhimu mkubwa mchezo wa kesho dhidi ya Sudan, utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa, Oktoba 27, mwaka huu nchini Mauritania, Stars ilifungwa bao 1-0, ambapo sasa ina kazi moja tu ya kupata ushindi wowote ili kujiweka katika nafasi nzuri kuelekea fainali hizo za mwakani.

“Tuna matumaini ya kushinda mchezo huu kwa sababu sisi tunataka tufuzu kwa kupitia njia hii, na kumbukumbu zinaonyesha mara zote mbili tulizocheza fainali za CHAN kulipitia mgongo wa Sudan,” alisema Ndimbo.

Mwaka 2019, Stars iliyokuwa chini ya Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije na Selemani Matola, iliwaondoa Sudan wakiwa nyumbani kwao na kufuzu kushiriki fainali za CHAN za mwaka huo.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *