TGNP yawajengea uwezo wanahabari kuhusu usawa wa kijinsia

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeandaa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari kutoka mikoa zaidi ya 10 nchini, yakilenga kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya usawa wa kijinsia.

Mafunzo hayo yamefanyika leo, Desemba 28, 2024, katika ofisi za TGNP jijini Dar es Salaam.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi, amesema kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuhamasisha jamii kuelewa na kuzingatia usawa wa kijinsia.

“Lengo letu ni kuhakikisha waandishi wa habari wanapata maarifa ya kina ya kuandika na kuripoti habari zinazogusa masuala ya kijinsia kwa usahihi na weledi,” amesema Liundi.

Mafunzo hayo yameongeza ufahamu kwa na wamejipanga kutumia vyombo vya habari kuelimisha jamii.

Katika mafunzo hayo, washiriki walipata fursa ya kujadili kuhusu ajenda ya Beijing iliyozinduliwa mwaka 1995 nchini China.

Ajenda hiyo ililenga kupigania haki za wanawake na kusisitiza usawa wa kijinsia.TGNP imeweka msisitizo wa kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuwa sehemu muhimu ya ajenda za kitaifa, huku ikihimiza ushirikiano wa vyombo vya habari katika kufanikisha malengo haya.

Washiriki wa mafunzo hayo walikubaliana kuwa kuendelea kuelimisha jamii kupitia habari za kijinsia ni hatua muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu na kuhakikisha haki kwa wote.

Mkutano wa Beijing, uliofanyika mwaka 1995, ulikuwa wa kihistoria kwa kuwa uliwakutanisha wanawake kutoka mataifa mbalimbali duniani kujadili masuala ya usawa wa kijinsia, haki za binadamu, na maendeleo ya wanawake.

Mkutano huo ulibeba maazimio yaliyolenga kuimarisha nafasi ya wanawake katika jamii na kupunguza pengo la kijinsia, ambayo bado yanahitajika kufanyiwa kazi kwa kina.

Katika kuelekea kumbukizi ya miaka 30 ya mkutano huo mwaka 2025, TGNP inasisitiza kuwa maazimio yake bado yana umuhimu mkubwa, na ni jukumu la kila mmoja kushiriki katika kuyatekeleza.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *