Mamlaka ya Mapato Tanzania, TRA, imekusanya shilingi trilioni 3.58 katika mwezi Machi 2026, sawa na ufanisi wa asilimia 107.6 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 3.32.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, makusanyo hayo yameifanya mamlaka hiyo kufikia jumla ya shilingi trilioni 9.31 katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026 (Januari hadi Machi), sawa na ufanisi wa asilimia 106.4 dhidi ya lengo la trilioni 8.75.
Amesema makusanyo hayo yanaonesha ukuaji wa asilimia 23.6 ikilinganishwa na shilingi trilioni 7.53 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2024/2025.
Aidha, katika kipindi cha miezi tisa kuanzia Julai 2025 hadi Machi 2026, TRA imekusanya shilingi trilioni 28.005 kati ya lengo la trilioni 26.773, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 16.5.
Mwenda ameongeza kuwa ufanisi katika usimamizi wa sheria za kodi umeimarika, ambapo uwiano wa kodi kwa gharama za makusanyo umefikia asilimia 2.41, huku uwiano wa kodi kwa pato la taifa ukikadiriwa kufikia asilimia 14.1 kutoka asilimia 13.7.




