Vijana kutoka Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya ambao ni wanufaika wa Mikopo ya asilimia kumi inayotolewa kwa Vikundi vya Vijana, Wanawake na wenye ulemavu kwenye Halmashauri zote nchini, wameishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwakwamua dhidi ya lindi la umaskini na kustawisha maisha yao kupitia mikopo hiyo nafuu na isiyokuwa na riba yoyote.
‎
‎Wakipigiwa mfano Vijana hao kutoka Vikundi Viwili vya Upendo Dispensary wanaomiliki Zahanati ya Evarest na kikundi cha Super Cargo, Vyote vya Wilayani Chunya, wameeleza namna ambavyo maisha yao yamebadilika, kukua kiuchumi na kushiriki katika ujenzi wa Taifa, wakimshukuru Rais Samia kwa kurahisisha na kuondoa vikwazo vilivyokuwepo awali katika utoaji wa Mikopo hiyo kwa Vikundi.
‎
‎Kulingana na Bw. George Augustine, tabibu kitaaluma na Mwanakikundi wa Upendo Dispensary, ameeleza kuwa Kikundi chao kina watu watano na walianza mchakato wa kupata mkopo wao mwaka 2022 na ilipofika mwanzoni mwa mwaka 2023, Halmashauri yao iliwapatia Mkopo wa Shilingi Milioni 39.5 na hivyo kuweza kukodi jengo na baadae kuzindua Zahanati yao.
‎
‎”Cha kwanza sisi wananchi tunafaidika sana na Vijana hawa, huduma zimekuwa karibu na wananchi na uzuri wa hawa Vijana wanajituma sana, wana lugha nzuri ya utu na wanaonesha jitihada kubwa sana za kujikwamua kimaisha.” Amesema Bi. Maria James, Mkazi wa Chunya na mnufaika wa Zahanati hiyo.
‎
‎Wakati wa hotuba yake Bungeni Mjini Dodoma mnamo Novemba 14, 2025, Rais Samia pamoja na mambo mengine aliahidi kuendelea kuitazama mikopo ya Asilimia 10 ili kuboresha upatikanaji wa mikopo hiyo kwa walengwa, akisema tamanio lake ni kuwa ifikapo 2030 Serikali yake iwe imetengeneza wawekezaji Vijana ambao watatoa ajira kwa wengine.
‎
‎Rais Samia akizingatia kuwa zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania ni Vijana, alisisitiza pia kuhakikisha Vijana wanapata nafasi ya kushiriki katika kujenga mustakabali mwema wa nchi, akiahidi kuweka kipaumbele kwenye ushirikishwaji wa Vijana, akitambua kuwa yapo majukwaa mengi ya kuwafikia Vijana ila bado shughuli zao zimekuwa zikififishwa na masuala ya siasa na hivyo kupoteza mvuto na ufanisi na ndio ikawa sababu ya kuunda Wizara maalum ya Vijana.




