Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Abubakar Zubeir Bin Ally, ametoa rai kwa waumini wa dini ya Kiislamu nchini, viongozi pamoja na Watanzania kwa ujumla kuwapuuza watu wanaoeneza chuki za kidini, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuishi kwa upendo, umoja na kuvumiliana kama yalivyo mafundisho ya Muhammad (S.A.W).
Mufti huyo alitoa kauli hiyo wakati akisoma tamko la maazimio ya kikao cha Baraza la Ulamaa kilichofanyika Machi 4, 2026 katika Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA). Katika tamko hilo aliwasihi Waislamu kutokubali kuchokozeka na watu wachache wanaoeneza ujumbe wa kumtukana Mtume, kuukashifu Uislamu na kuibeza dini hiyo.
“Tunaamini wanaofanya hayo si Wakristo wala watu wa dini nyingine yeyote, bali ni watu wenye nia ovu ya kutuchonganisha ili tugombane na kusababisha mtafaruku kati yetu na dini nyingine pamoja na jamii kwa ujumla. Niwasihi Waislamu wasiingie kujibizana kwa sababu watu hao wanataka kueneza chuki na fitna dhidi ya dini nyingine,” amesema Mufti.
Aidha, amewataka Waislamu wote nchini wakiwamo Masheikh, wanazuoni, Maustadh, maimamu, waalimu wa dini pamoja na jamii kwa ujumla kuendelea kuishi kwa upendo, kuvumiliana na kudumisha umoja wa kitaifa uliodumu kwa muda mrefu nchini.
“Mtume Muhammad (S.A.W) aliishi na wasiokuwa Waislamu kwa wema na alishirikiana nao kwa amani,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Mufti huyo amewataka Waislamu na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwamo COVID-19, Hepatitis, Dengue Fever na Cholera kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na serikali.
Pia amewatakia Waislamu wote wanaoendelea na ibada ya kufunga katika Ramadan muendelezo mwema wa mfungo huo mtukufu.




