TVLA yang’ara Nanenane 2025, yanyakua tuzo tano Kitaifa na Kanda

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imepata heshima kubwa kitaifa baada ya kutunukiwa tuzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuibuka mshindi wa kwanza miongoni mwa wakala wa serikali wanaotoa huduma bora na zenye tija kwa sekta ya mifugo nchini.

Ushindi huo ulipatikana kupitia maonesho ya kilimo ya Nanenane Kitaifa yaliyofanyika katika Uwanja wa Nzuguni, mkoani Dodoma kuanzia Agosti 1–8, 2025.

Mbali na mafanikio hayo ya kitaifa, TVLA pia iliibuka kinara katika maonesho ya Nanenane katika ngazi za kanda:

  • Kanda ya Ziwa Magharibi – TVLA ilishika nafasi ya kwanza kwenye kipengele cha Taasisi za Uchunguzi Maabara, tuzo iliyokabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, katika maonesho yaliyofanyika Uwanja wa Nyamhongolo, Mwanza.
  • Kanda ya Kusini – Iliibuka mshindi wa tatu kwenye kipengele cha Taasisi za Huduma za Utafiti, tuzo ikitolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Saidi Jafo, katika maonesho ya Uwanja wa Ngongo, Lindi.
  • Kanda ya Ziwa Mashariki – TVLA ilipata nafasi ya pili kwenye kipengele cha Taasisi za Umma, tuzo ikikabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, katika maonesho yaliyofanyika Uwanja wa Nyakabindi, Simiyu.
  • Kanda ya Magharibi – Ilishika nafasi ya pili kwenye kipengele cha Taasisi za Serikali zinazotoa Huduma za Uzalishaji, tuzo hiyo ikitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, IGP (Mst.) Balozi Simon Sirro, katika maonesho yaliyofanyika Uwanja wa Fatma Mwasa, Tabora.

Akizungumzia ushindi huo, Mtendaji Mkuu wa TVLA, Dkt. Stella Bitanyi, alisema:

“Kupata tuzo tano katika ngazi ya kitaifa na kanda ni jambo la heshima na fahari kwa TVLA. Ushindi huu ni matokeo ya bidii ya watumishi wetu, uwekezaji wa serikali, na uongozi makini wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya mifugo. Tuzo hizi zinatupa hamasa ya kuendelea kuboresha huduma zetu za kitaalamu, kuendeleza ubunifu katika tafiti na uchunguzi wa magonjwa, pamoja na kusaidia wafugaji kuongeza tija na kipato.”

Dkt. Bitanyi aliongeza kuwa TVLA imejidhihirisha kama nguzo muhimu ya maendeleo ya sekta ya mifugo nchini na itaendelea kuwekeza kwenye teknolojia za kisasa ili kuhakikisha Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi zenye mifumo bora ya afya ya wanyama barani Afrika.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *