
TIMU ya Soka ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), inatarajia kukutana na Senegal katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayochezwa leo, nchini Morocco.
Twiga Stars inacheza mechi ya pili ya kirafiki ya kimataifa, baada ya mchezo wake uliotangulia dhidi ya Morocco, kumalizika kwa kupokea kichapo cha mabao 4-1.
Bao pekee la Twiga Stars katika mechi hiyo ya juzi, lilifungwa na Enekia Lunyamila, ambaye anacheza soka la kulipwa katika Klabu ya Mazatlan iliyoko Mexico.
Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Hilda Masanche, alisema jana, ameyafanyia kazi makosa waliyofanya katika mechi ya kwanza, lakini pia ameimarisha katika maeneo ambayo walifanya vizuri.
Masanche alisema timu yake imepata kipimo kizuri kwa ajili ya kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON), zitakazofanyika kuanzia Julai 6 hadi 26, mwakani.


Kocha huyo alisema wapinzani wao Morocco wana uzoefu, lakini amewapongeza wachezaji wake kwa kuonesha kiwango kizuri licha ya kukubali kufungwa.
“Kiufundi tulitumia mechi ya jana (juzi), kama darasa na namna tutakavyojiimarisha kuelekea michuano ya WAFCON, ni mechi nzuri kwetu kwa ajili ya kujifunza, tunaangalia tulipokosea, ili kuparekebisha lakini kulinda kile ambacho tulifanya vizuri,†alisema Masanche.
Aliongeza mechi ya leo dhidi ya Senegal wanatarajia utakuwa mchezo wa kutumia nguvu na akili zaidi, kwa sababu ya aina ya uchezaji wa mpinzani wao.
Alisema pia bado wanaendelea kuwajenga wachezaji wao ambao kwa sasa kuna mchanganyiko wa nyota wapya na wale wazoefu katika kikosi hicho.
Chanzo: Nipashe