Shinyanga imetapika, ndiyo maneno machache yanayotosha kuelezea uhalisia wa maelfu ya wananchi waliofurika katika Uwanja wa CCM Kambarage, kuhudhuria mkutano wa kampeni za Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan.
Umati huo wa maelfu ya wananchi, unaufanya Mkoa wa Shinyanga, uvunje rekodi ya mikoa mingine, iliyoshuhudiwa ikifurika watu katika mikutano ya kampeni za urais za Dkt Samia, tangu alipoanza Agosti 28, mwaka huu.


Hata hivyo, mafuriko hayo ya wananchi katika viwanja hivyo mkoani Shinyanga, yanakuja wakati ambao, mikutano ya kampeni za urais ya Dkt Samia aliyoifanya katika mikoa 21 ya awali, imeandika rekodi ya kuhudhuriwa na wananchi milioni 14.62.
Idadi hiyo ya waliohudhuria, ni sawa na asilimia 23.67 ya Watanzania wote, ukiacha wale waliofuatilia mikutano hiyo, kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ambao ni milioni 31.6, sawa na asilimia 51.2 ya Watanzania wote.


Kwa maneno mengine, mikutano ya kampeni ya Dkt Samia katika mikoa 21 ya awali, ukitoa Kanda ya Ziwa inayohusisha Shinyanga, imehudhuriwa na kufuatiliwa na asilimia 74.9 ya Watanzania.
Hii inamaanisha robo tatu ya Watanzania wamemfuatilia Dkt Samia, jambo linaloashiria ushindi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.

