Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCDF) limekubali kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa awamu ya pili ya Programu ya LoCAL, ambayo inalenga kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kupitia programu hiyo, Serikali inatekeleza mradi wenye thamani ya dola milioni 11, unaotekelezwa katika halmashauri 18 za Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kuongeza uhimilivu wa jamii dhidi ya athari za tabianchi.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika mkutano kati ya Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdallah Hassan Mitawi, na Afisa wa UNCDF, Damiano Borgogno, pembezoni mwa Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) unaofanyika jijini Belem, Brazil.
Aidha, katika mazungumzo hayo UNCDF imeonesha utayari wa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika maeneo mengine yanayohusiana na hifadhi endelevu ya mazingira.
Naibu Katibu Mkuu Mitawi amelishukuru shirika hilo kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kusimamia mazingira, ikiwemo kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi. Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kupata miradi zaidi itakayosaidia kukuza maendeleo endelevu ya mazingira nchini.




