Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP Tanzania) pamoja na Serikali ya Uingereza kupitia Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO) imetoa zaidi ya TSh milioni 70 kama mtaji wa awali (seed funding) kwa biashara bunifu zilizoanzishwa na wanafunzi wa vyuo vikuu, ikiwa ni sehemu ya msimu wa pili wa Mpango wa Kubadilishana Ujuzi miongoni mwa wahadhiri wa vyuo vikuu Afrika ya Mashariki, uliofanyika kwa siku tatu katika chuo cha Indian Institute of Technology Madras Zanzibar (IIT Madras) kampasi ya Zanzibar.
Mpango huo uliwakutanisha wabunifu wanafunzi, viongozi wa vyuo vikuu, wakufunzi na wadau wa mfumo wa ubunifu ili kuimarisha nafasi ya vyuo vikuu kama injini za ujasiriamali na ubunifu. Mpango huu unaendeleza mafanikio ya toleo la kwanza lililojulikana kama RISE 4.0, na unaendelea kuwasaidia wabunifu vijana kubadilisha mawazo yaliyotokana vyuoni kuwa biashara halisi zinazoweza kukua.
Mpango huo unatekelezwa na UNDP kupitia Mradi wa FUNGUO, kwa ushirikiano na Serikali ya Uingereza kupitia Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO). Ushirikiano huu unalenga kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini Tanzania kwa kuwaunganisha wanafunzi na ushauri elekezi, fursa za ufadhili, na mazingira yatakayowezesha mawazo yao kukua na kuwa biashara endelevu.




Kabla ya kutangazwa kwa washindi, timu za wanafunzi zilipata mafunzo na ushauri wa kina kutoka kwa wataalamu wa vyuo vikuu shiriki pamoja na wadau wa mfumo wa ubunifu. Mafunzo hayo yalijikita katika uundaji wa mawazo ya biashara, kukuza maendeleo ya biashara changa, mikakati ya kuingiza ubunifu sokoni, na namna ya kujenga biashara zinazoweza kupanuka na kushindana sokoni.
Biashara bunifu sita ziliingia fainali za mpango wa mwaka huu, kwa mpangilio wa mshindi wa kwanza mpaka wa sita, zilikuwa Vestis, Naarad, CropIQ, Carbon Trace, Ecofy, na Power Taka.
Mshindi wa jumla, Vestis, biashara bunifu iliyoanzishwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ilipokea TSh milioni 15 kama mtaji wa awali. Jukwaa hilo linalenga kurahisisha ununuzi na uuzaji wa nguo mtandaoni, likiwawezesha watumiaji kuokoa muda na gharama za usafiri zinazotumika kwenda sokoni.
Mbali na mtaji huo wa awali, biashara hizo bunifu zitapata msaada endelevu kupitia fursa za kuwasilisha mawazo yao kwa wawekezaji, mafunzo ya masoko na uendeshaji wa biashara, ushauri elekezi, pamoja na fursa za kujenga mitandao na wadau wa mfumo wa ubunifu na wawekezaji watarajiwa.
Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo, Bw. Joseph Manirakiza, Meneja wa Mpango wa FUNGUO katika shirika la UNDP Tanzania, alisema kuwa toleo la pili la mpango huu linaonesha dhamira endelevu ya UNDP nchini katika kukuza ubunifu miongoni mwa wajasiriamali vijana nchini Tanzania.






“Msimu huu wa pili wa Mpango wa Kubadilishana Ujuzi miongoni mwa wahadhiri wa vyuo vikuu Afrika ya Mashariki unajenga kuhusu mafanikio ya toleo la kwanza lililojulikana kama RISE 4.0. Kupitia Mpango wa FUNGUO, UNDP imekuwa ikiunga mkono ukuaji wa ubunifu unaotokana na vyuo vikuu nchini Tanzania. Mpaka sasa, zaidi ya biashara bunifu 70 zinazoongozwa na wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali zimefaidika na mpango huu. Kwa kushirikiana na wadau kama Serikali ya Uingereza, tunalenga kupanua wigo wa mpango huu na kuongeza manufaa yake kwa kuwasaidia wabunifu vijana wengi zaidi kubadilisha mawazo yao kuwa biashara endelevu,” alisema.
Akizungumza pia katika tukio hilo, Dkt. Erasto Mlyuka, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uendelezaji na Uhawilishaji wa Teknolojia (COSTECH), alithibitisha dhamira ya serikali ya kuendelea kuunga mkono ubunifu na ujasiriamali miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
“Serikali inaunga mkono kwa dhati programu kama hizi zinazochochea ubunifu na ujasiriamali miongoni mwa wanafunzi. Vyuo vikuu vinapaswa kubadilisha mbinu zao kwa kuwajengea wanafunzi uwezo na ujuzi wa ujasiriamali ili wanapohitimu wawe tayari kuanzisha kampuni zao badala ya kutafuta ajira pekee. Nimevutiwa sana na mawazo yaliyowasilishwa na wanafunzi hawa, ikiwemo ubunifu katika sekta mpya kama suluhisho za kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa. Serikali itaendelea kuunga mkono mijadala na mipango ya aina hii,” alisema.






Kwa niaba ya timu iliyoshinda, Kelvin Erasto, mwakilishi wa kampuni changa ya Vestis, alisema kuwa kiasi hiko cha fedha kitawezesha biashara hiyo kupanua shughuli zake na kuwafikia watumiaji wengi zaidi.
“Msaada huu utatusaidia kupanua jukwaa letu na kurahisisha shughuli zetu za kila siku za biashara tunapolenga kuwafikia watu wengi zaidi. Pia tunatarajia kuendelea kupata mafunzo na ushauri kutoka kwa wataalamu wa vyuo vikuu ili kuimarisha mtindo wetu wa biashara na kuharakisha ukuaji wake,” alisema.
Ukifanyika chini ya kaulimbiu “Vyuo Vikuu kama Injini za Ubunifu: Kujenga Njia Endelevu kutoka Maarifa mpaka Biashara,” mpango huu unaviweka vyuo vikuu kama nguzo muhimu za ubunifu, uendelezaji wa teknolojia na ukuaji wa biashara.
Mpango huo uliwakutanisha wahadhiri kutoka vyuo vikuu, watunga sera na wadau wa mfumo wa ubunifu kwa siku tatu mfululizo kuanzia Machi 4 hadi 6 katika chuo cha IIT Madras kampasi ya Zanzibar ili kujadili namna taasisi za elimu ya juu zinavyoweza kuwa na mchango mkubwa zaidi katika uanzishaji wa biashara bunifu, uendelezaji wa tafiti kibiashara, na ukuaji wa biashara zinazoendeshwa na ubunifu nchini Tanzania na Afrika Mashariki.
Kwa kuunganisha ujenzi wa uwezo, ushauri elekezi na mtaji wa awali, mpango huu unalenga kuimarisha mlolongo wa biashara bunifu zinazozaliwa vyuoni ambazo zina uwezo wa kuzalisha ajira, kutatua changamoto za maendeleo, na kuchangia ukuaji wa uchumi wa ubunifu nchini Tanzania.








