Uongozi wa klabu, ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Crescentius Magori pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu, Murtaza Mangungu, umekutana na benchi la ufundi pamoja na wachezaji kwa lengo la kuweka mikakati thabiti kuelekea msimu mpya wa 2025/26.
Katika kikao hicho, viongozi walitoa maelekezo na msisitizo kuhusu nidhamu, mshikamano, na uwajibikaji ndani ya kikosi, wakisisitiza umuhimu wa kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa umakini.




Pia walieleza malengo makuu ya klabu kwa msimu ujao, yakiwemo kufanya vizuri katika mashindano ya ndani na ya kimataifa, kuhakikisha timu inacheza soka la ushindani na la kuvutia, pamoja na kuendeleza vipaji vya wachezaji chipukizi.
Aidha, kikao hicho kilikuwa nafasi ya wachezaji na benchi la ufundi kutoa maoni yao kuhusu maandalizi ya msimu, changamoto zilizopo, na maeneo yanayohitaji kuimarishwa.

Viongozi waliahidi kutoa ushirikiano wa karibu, kuhakikisha mazingira bora ya kazi, vifaa vya kisasa na motisha kwa wachezaji ili kufanikisha safari ya mafanikio ya klabu.





