Sunday, December 7, 2025
spot_img
HomeHabariViongozi wa Dini Mara watoa wito kudumishwa amani kipindi cha uchaguzi

Viongozi wa Dini Mara watoa wito kudumishwa amani kipindi cha uchaguzi

Viongozi wa dini mkoani Mara wameitaka jamii kudumisha amani katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, na kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Wakizungumza kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo, viongozi hao wamesema kumekuwepo na watu wachache wanaosambaza taharuki miongoni mwa wananchi, na kuonya kwamba vitendo hivyo vinaweza kuhatarisha utulivu wa nchi.

Wameiomba Serikali kuchukua hatua madhubuti kuwabaini na kuwachukulia hatua wale wote wanaohatarisha amani, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwalinda wananchi wakati wa mchakato wa uchaguzi.

Akizungumzia umuhimu wa umoja na amani, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema msingi wa mshikamano wa taifa ni jamii kuishi kwa upendo na amani.

“Viongozi wa dini wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha waumini kuhusu umuhimu wa kupiga kura na kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa amani,” alisema Nyalandu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Canali Evance Mtambi, alisema vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda raia na mali zao, na kuhakikisha mipaka ya nchi inabaki salama.

Alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuepuka vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani na badala yake wakumbatie umoja na mshikamano wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments