Vodacom yazindua msimu wa 4:Digital Accelerator, Biashara bunifu 15 zateuliwa kushiriki  Design Sprint

  • Kufundishwa ujasiriamali na Wataalamu wa Kimataifa kutoka Marekani

Vodacom Tanzania PLC, kwa kushirikiana na Huawei Tanzania, leo imezindua rasmi Msimu wa 4 wa Vodacom Digital Accelerator (VDA), hatua nyingine katika kusaidia ubunifu na ujasiriamali nchini .

Mwaka huu, biashara bunifu 15 zimechaguliwa kushiriki katika programu ya siku 5 ya Design Sprint, itakayoendeshwa na wataalam wa kimataifa kutoka programu ya MassChallenge ya nchini Marekani.

Lengo la Design Sprint ni kuboresha  biashara zinazochipukia, kuimarisha ufanisi wa bidhaa sokoni na kuongeza maandalizi yao kwa ajili ya kuvutia uwekezaji. Kati ya hizi, biashara 10 zenye uwezo mkubwa wa kufanikiwa zitachaguliwa kwa safari ya miezi 3 ya kuendelezwa, ambapo zitapata ushauri wa kitaalam, msaada wa maendeleo ya biashara, na fursa mahususi za kufikia masoko ya ndani na ya kimataifa.

Msimu wa 4 wa VDA unaendeshwa kupitia ushirikiano wa kimkakati unaoendelea kati ya Vodacom na Huawei, jambo litakalowezesha wabunifu hao kushiriki kwenye safari ya kujifunza nchini China mwezi Juni. Wakati wa ziara hiyo ya kimataifa, wabunifu hao watakutanishwa na kampuni kubwa za teknolojia za nchini China, ili kujifunza  mifumo ya ubunifu wa kisasa na pia kuwasilisha bunifu  zao mbele ya wawekezaji binafsi na mashirika.

Katika hatua kubwa ya kuwaendeleza  wajasiriamali chipukizi , msimu huu utakuwa na uwekezaji wa fedha taslimu zitatolewa kwa biashara tatu bora, ili kusaidia kukuza bunifu  zao na hivyo kuwaongezea uwezo wa ushindani ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

“VDA ni jukwaa la ukuzaji wa kizazi kijacho cha wavumbuzi wa Kitanzania. Na kwa mara nyingine tunachanganya ubunifu wa ndani na uzoefu wa kimataifa tukiwasaidia vijana wabunifu katika kujenga biashara zinazoweza kupanuka, kupata uwekezaji na kuingia kwenye majukwaa ya kimataifa,” alisema Zuweina Farah, Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano  wa Vodacom Tanzania.

Tangu kuanzishwa kwake, Vodacom Digital Accelerator imewezesha zaidi ya biashara chipukizi 75 nchini kwa kuwapatia nyenzo, mtaji na kuwakutanisha na wajasiriamali na makampuni makubwa iliyowawezesha  kukua na kustawi. Msimu wa 4 unaendeleza urithi huu, kwa dhamira mpya ya ujumuishwaji wa kidijitali, uhifadhi wa baiyoanuai, ujasiriamali wa vijana na uwezeshaji wa kiuchumi.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *