Waandishi wa habari nchini wametakiwa kuzingatia misingi, maadili na miiko ya taaluma hususan kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ili kutoa taarifa sahihi na zisizoegemea upande wowote kwa ustawi wa jamii na Taifa.

Wito huo umetolewa Agosti 14, 2025 jijini Dar es Salaam katika mafunzo ya siku moja ya Uandishi wa Habari za Uchaguzi yaliyoandaliwa na Kampuni ya Media Brains kwa kushirikiana na Taasisi ya Konrad Adenauer Stiftung (KAS).
Mafunzo hayo yaliwahusisha waandishi kutoka vyombo mbalimbali na yalijikita katika uelewa wa sheria mpya za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Mwakilishi Mkazi wa KAS, Peter Koch, alisema vyombo vya habari ni nguzo muhimu za demokrasia, vikihusisha wananchi na viongozi, hivyo waandishi wanapaswa kuepuka upendeleo, kutoa habari sahihi, kuheshimu faragha na kuepuka lugha ya chuki.





Alisisitiza umuhimu wa mafunzo ya namna bora ya kuripoti ili kukuza uwajibikaji na ushiriki wa wananchi katika uchaguzi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Media Brains, Jesse Kwayu, alisema waandishi wanapaswa kutumia kalamu zao kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki uchaguzi na kuchagua viongozi bora.
Aliongeza kuwa demokrasia hudhoofika pale uandishi unapokuwa wa uchochezi au wa upande mmoja, na kusisitiza kutoa nafasi sawa kwa wagombea wanawake na wanaume.
Mkurugenzi Mwenza wa Media Brains, Absalom Kibanda, aliwataka waandishi kufuata maadili, miiko na sheria za uchaguzi, kuepuka ushabiki wa kisiasa, na kuzingatia usalama wao wanaporipoti masuala ya kisiasa.
















