Sunday, October 12, 2025
spot_img
HomeElimuWaandishi wa sheria Tanzania waongezewa ujuzi kwa teknolojia ya Uingereza

Waandishi wa sheria Tanzania waongezewa ujuzi kwa teknolojia ya Uingereza

Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria,  wamefanya ziara ya mafunzo nchini Uingereza, ikiwa ni sehemu ya ushiriki wao katika Mkutano wa Jumuiya ya Waandishi wa Sheria wa Jumuiya ya MadolaKanda ya Ulaya. 

Ziara hiyo ambao ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Ofisi hiyo wa kuboresha utendaji wake kupitia mafunzo ya kimataifa, ubadilishanaji wa uzoefu, na ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika nyanja ya uandishi wa sheria na urekebu wa sheria, imelenga kujifunza mbinu, mifumo na teknolojia mpya za uandishi na urekebu wa sheria ili kuboresha utendaji wa ofisi hiyo muhimu nchini Tanzania.  

Akizungumza kuhusu ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Divisheni ya Urekebu wa Sheria, Utafiti na Mafunzo wa Ofisi hiyo, Rehema Katuga, amesema safari hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwani imewapa fursa ya kuona kwa vitendo namna wenzao wa Uingereza wanavyotekeleza majukumu yao katika nyanja ya uandishi wa sheria kwa kutumia mifumo ya kisasa na mipango madhubuti ya mafunzo.

“Tulijifunza kwa kina jinsi wanavyofanya kazi kama taasisi huru inayojitegemea lakini yenye uhusiano wa karibu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hii imetupa mwanga juu ya namna tunavyoweza kuboresha mifumo yetu nchini,” amesema Rehema.

Rehema amesema kupitia ziara hiyo, maafisa hao waliweza kujifunza pia kuhusu namna nchi hizo zinavyoshughulikia masuala ya urekebu wa sheria na jinsi mifumo yao ya utunzaji wa kumbukumbu inavyowezesha urahisi wa kupata taarifa za kisheria kwa wananchi.

“Tunarejea nchini tukiwa na maono mapya, tumepata somo la namna tunavyoweza kuboresha Ofisi yetu kwa kuimarisha matumizi ya teknolojia, kubuni mpango wa mafunzo endelevu kwa waandishi wa sheria, na kuhakikisha kuwa taratibu zote za uandishi wa sheria zinakuwa wazi, shirikishi na zenye ufanisi,” amesema Rehema.

Alfred Nyaronga ambaye ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA katika Ofisi hiyo, amesema timu hiyo pia ilitembelea Ofisi ya Taifa ya Kumbukumbu ya Nyaraka ambako walijifunza kuhusu mfumo wa kidigitali wa Lawmaker, unaotumika katika maandalizi, marekebisho na urekebu wa sheria nchini Uingereza.

Amesema mfumo wa Lawmaker unawawezesha wadau wote wa uandishi wa sheria kuanzia wizara, bunge, ofisi ya mwandishi wa sheria, hadi mpigachapa wa serikali  kufanya kazi kwa pamoja katika jukwaa moja la kidigitali ambapo mswada unaweza kupitiwa, kurekebishwa, na kupitishwa hatua kwa hatua ndani ya mfumo huo hadi unapokuwa sheria kamili.

Nyaronga amesema mfumo huo pia hutumika katika urekebu wa sheria kwa kuruhusu sheria zilizofanyiwa marekebisho kuunganishwa moja kwa moja, hivyo kumwezesha mwananchi au mdau yeyote kupata toleo la kisasa la sheria husika mara moja na hivyo kunaongeza uwazi, ufanisi na upatikanaji wa taarifa za kisheria kwa umma, jambo ambalo tungependa kuona linatekelezwa pia hapa nchini.

Bavoo Junus, ambaye ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha uhakiki ubora kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria,      amesema kuwa pamoja na nchi za magharibi kupiga hatua kubwa kwenye matumizi ya teknolojia katika uandishi wa sheria lakini pia  wameshughulikia changamoto mbalimbali zinazoletwa na matumizi ya mifumo hiyo na kuongeza ufanisi.

Bavoo amesema jambo lingine muhimu ambalo wamejifunza kwenye ziara hiyo ni mafunzo kuhusu jinsi wanavyosimamia shughuli za uandishi wa sheria na kuwajengea uwezo waandishi wapya kupitia mafunzo ya ndani.

“Wenzetu wameweka utaratibu wa kuwa na mafunzo ya ndani ili kusaidia Waandishi wachanga na wageni kwenye fani hiyo, ambapo waandishi wa sheria wenye uzoefu hupewa wajibu wa kuwafundisha waandishi wapya kwa kipindi cha mwaka au zaidi hivyo mfumo huu wa ushauri na mafunzo ya vitendo umekuwa na matokeo makubwa katika kukuza ujuzi na kuimarisha ubora wa kazi,” amesema Bavoo.

Wataalamu hao kutoka Tazania, pia walipata fursa ya kutembelea Bunge la Uingereza, ambapo walijifunza kuhusu utendaji wa kila chombo cha kutunga sheria, utaratibu wa vikao, na historia ya Bunge hilo lenye asili ndefu katika demokrasia ya kisheria.

Uzoefu huo umefungua ukurasa mpya katika kuboresha mifumo ya ndani, ikiwamo matumizi ya teknolojia katika uandishi wa sheria, Urekebu wa sheria,Ufasili wa sheria na usimamizi wa kumbukumbu.     

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments