Wadau, wanataaluma, na wanafunzi wameshiriki kongamano la 11 la kitaaluma (Convocation) juu ya uwezeshaji na ubunifu katika kubadilisha elimu kuwa fursa.

Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam, Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Prof. Sotco Komba, alisema kuwa kongamano hili limekuwa fursa kwa wanafunzi kujifunza masuala ya ubunifu, ambapo katika maisha ya sasa ubunifu ni kichocheo cha maendeleo katika jamii. Kupitia mada kuu iliyowasilishwa, wanafunzi wameelewa dhana nzima ya ubunifu.
Dkt. Haruna Makandi, Mratibu Tafiti Mwandamizi kutoka Idara ya Maendeleo ya Teknolojia katika Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH), alisema kuwa wanafunzi wanapaswa kuendelea kuwa wabunifu na kushirikisha wadau mbalimbali pamoja na taasisi zinazojihusisha na ubunifu. Hii itawawezesha kukutanishwa na wawekezaji pamoja na kupewa miongozo ya kulinda bunifu zao.




Ni utamaduni wa Chuo cha Ustawi wa Jamii kufanya kongamano hili kila mwaka kabla ya mahafali, ambapo kwa mwaka 2024 kongamano hili linatarajiwa kuwa jukwaa la kukuza uwezo wa wanafunzi na kujenga mahusiano kati ya elimu na fursa za maendeleo.


