Wakazi Chalinze wapatiwa huduma ya macho bure

Wananchi wamehimizwa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara, hususan uchunguzi wa macho, ili kuzuia matatizo ya kiafya yanayoweza kujitokeza na pia kupunguza gharama kubwa za matibabu.

Wito huo umetolewa na Dk. Nelson Swai, daktari bingwa wa magonjwa ya macho kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), wakati wa kambi ya uchunguzi wa macho inayoendelea kutolewa bure katika Hospitali ya Wilaya ya Msoga, iliyopo Chalinze mkoani Pwani.

Dk. Swai alisema kuwa kambi hiyo ya huduma ya macho imeandaliwa kwa ushirikiano kati ya MUHAS na Taasisi ya Vision Care kutoka Korea Kusini, ikiwa na lengo la kuwafikia wananchi hasa wa maeneo yenye uhitaji mkubwa wa huduma za afya.

“Tangu kambi hii ianze siku ya jana, tayari tumewahudumia wagonjwa 330. Kati yao, wagonjwa 30 wamefanyiwa upasuaji wa macho na wengine wamepewa dawa kulingana na matatizo yao,” amesema Dk. Swai.

Amesisitiza umuhimu wa watu wote, bila kujali hali yao ya afya, kufanya uchunguzi wa macho angalau mara moja kwa mwaka.

“Kitaalamu, huhitaji kungoja hadi uanze kupata matatizo ya kuona ndipo uende hospitali. Magonjwa kama presha ya macho (glaucoma) yanaweza kuanza bila dalili zozote, na yakigundulika kuchelewa huweza kusababisha upofu wa kudumu,” ameeleza Dk. Swai.

Ameongeza kuwa huduma za macho hazipaswi kuwalenga wazee pekee, bali watoto pia wanapaswa kupimwa ili matatizo yachukuliwe hatua mapema kabla hayajakomaa.

Aidha, amesema kambi hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kutoa huduma muhimu za afya kwa jamii ambazo kwa kawaida hupata ugumu wa kupata huduma hizo.

Kwa upande wao, wananchi waliohudumiwa wametoa shukrani kwa MUHAS na washirika wake kutoka Korea Kusini.

“Nashukuru MUHAS na madaktari wetu wa macho kwa moyo wao wa kujitolea. Nimefanyiwa upasuaji wa jicho na naendelea kupona vizuri,” amesema Hasnat Salim, mkazi wa Mdaula.

Naye William Tundameja, mkazi wa Pingo, alisifu huduma hiyo na kuomba iwe endelevu:

“Nimepatiwa uchunguzi wa macho na dawa bure. Huduma ni bora sana, na tunatarajia huduma hii iendelee kuwafikia wananchi wengine wasio na uwezo wa kumudu gharama za matibabu,” amesema.

Kambi hiyo inatarajiwa kuendelea hadi Alhamisi ya wiki hii, huku waandaaji wakisisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha jamii nyingi zaidi zinanufaika.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *