Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu imezindua rasmi mpaka wa makatazo ya kufanya shughuli za kibinadamu na kibiashara ndani ya mita 60 kutoka kandokando ya Mto Mpiji, uliopo Mtaa wa Bunju B, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, ikiwa ni hatua muhimu ya kulinda na kuhifadhi vyanzo vya Maji.
Uzinduzi huo umefanyika kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mheshimiwa Saad Mtambule, pamoja na viongozi wa serikali za mitaa na wadau wa mazingira wakiwemo wakandarasi na machepe, ikiwa ni sehemu ya juhudi za pamoja za kuimarisha ulinzi wa rasilimali za maji katika eneo hilo.




Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni amesema uwekaji wa mpaka huo wa makatazo unalenga kudhibiti shughuli zinazoweza kuhatarisha vyanzo vya maji, zikiwemo ujenzi holela, kilimo kandokando ya mito, uchimbaji wa mchanga na vitendo vingine vinavyosababisha uharibifu wa kingo za mito na kuathiri mazingira.
Katika kuunga mkono juhudi hizo za uhifadhi wa mazingira, zoezi la upandaji miti pia limefanyika ambapo jumla ya miti 500 ya matunda pamoja na miti rafiki kwa mazingira ya mito imepandwa kandokando ya Mto Mpiji. Lengo ni kuimarisha kingo za mto, kupunguza mmomonyoko wa udongo, kulinda mfumo wa ikolojia na kupunguza shughuli za kilimo zinazotumia kemikali karibu na chanzo cha maji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kidakio cha Pwani kutoka Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu amewahimiza wananchi kuzingatia sheria na kanuni za uhifadhi wa rasilimali za maji kwa kuepuka kufanya shughuli ndani ya eneo la hifadhi ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji. Amesisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kulinda rasilimali hiyo muhimu kwa ustawi wa Jamii na maendeleo ya Taifa.









