Wananchi wa jijini Dar es Salaam wameendelea kuhamasishwa kuhusu suluhisho la mapishi kwa kutumia nishati ya umeme, ikiwa ni sehemu ya Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji wa Upishi wa Umeme (eCooking) iliyoanzishwa rasmi Juni 13, 2025.

Kampeni hiyo inaratibiwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Programu ya Huduma za Nishati za Kisasa za Kupikia (MECS) na Shirika la Maendeleo la Uingereza (UK International Development), kwa lengo la kuhamasisha mabadiliko ya tabia ili kaya nyingi zaidi nchini ziachane na matumizi ya kuni na mkaa ambayo yana madhara kwa afya na mazingira.
Katika kuimarisha utekelezaji wa kampeni hiyo, washirika wa maendeleo wamekabidhi magari mawili kwa Wizara ya Nishati, yatakayotumika kwa shughuli za utoaji elimu na ufuatiliaji katika maeneo mbalimbali nchini.
Kampeni ya eCooking inalenga kufikisha ujumbe kwa Watanzania kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi, salama na rafiki kwa mazingira katika shughuli za kila siku za upishi.


