Wanawake wanaojishughulisha na biashara ya usambazaji wa bidhaa za Phytoscience, ambazo zinasaidia kuimarisha seli za mwili, wametakiwa kutumia vyema fursa za kiuchumi zilizopo katika sekta hiyo ili kujiongezea kipato na kujikwamua kiuchumi.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Kiuchumi Wanawake jijini Dar es Salaam, Rehema Sanga, alitoa wito huo wakati akizungumza na wanawake wa taasisi ya Phytoscience, wakiongozwa na Mkurugenzi Susan Moshi, katika mkutano maalum wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Sanga alisisitiza kuwa wanawake wana nafasi kubwa ya kufanikisha maendeleo yao binafsi na jamii zao kupitia biashara ya bidhaa za afya, ikiwa watazitumia fursa zilizopo kwa ubunifu na ufanisi.
“Sekta ya bidhaa za afya kama hizi za Phytoscience inatoa fursa kubwa kwa wanawake kujiongezea kipato. Ni muhimu tushirikiane, tujitume, na tujifunze mbinu bora za biashara ili tuweze kufanikisha maendeleo yetu ya kiuchumi,” alisema Sanga.
Naye Mkurugenzi wa Phytoscience, Susan Moshi, aliwatia moyo wanawake kushiriki kwa wingi katika biashara hiyo kwa kuwa ina faida kubwa na inaweza kusaidia kuinua viwango vya maisha ya familia zao. Alisisitiza umuhimu wa mtandao wa wanawake kushirikiana ili kuimarisha nafasi yao katika sekta ya afya na biashara.
Maadhimisho hayo yalitoa nafasi kwa wanawake kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu mpya za ujasiriamali, na kuhamasishana katika kujenga uchumi endelevu kupitia sekta ya bidhaa za lishe na afya.