Wastaafu wanaopokea Pensheni kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) wamekumbushwa kuwa endapo mstaafu anahitaji kufanya mabadiliko ya majina yake anapaswa kufanya hivyo ndani ya miezi mitatu ya kustaafu kwake.

Hayo yameelezwa na Meneja wa PSSSF Kanda ya Ziwa Mashariki, Rajabu Kinande, wakati akitoa elimu ya Hifadhi ya Jamii kwenye Maonesho ya Kimataifa ya 32 ya Nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya Nyamuhongolo jijini Mwanza.
“Lengo ni kudhibiti udanganyifu, kuepuka utofauti wa taarifa za mstaafu baina ya Mfuko na taasisi inazoshirikiana nazo.” amefafanua Kinande.
Aidha, amewaasa wastaafu kutunza taarifa zao na daima ziwe ni siri yao kwani inasaidia kudhibiti vitendo vya kutepeliwa na kuepuka usumbufu.
“Tunawashauri wastaafu wetu kutopokea maelekezo kutoka kwa watu wasiowafahamu na endapo wana jambo lolote wanalohitaji ufafanuzi, wawasiliane moja kwa moja na ofisi za Mfuko ambazo zimeenea nchi nzima Tanzania bara na Zanzibar.” amesisitiza Kinande.






