Wataalam waonywa wanaotumia chanjo kujinufaisha kibiashara

Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa onyo kwa maafisa na watalaam wanaotekeleza Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo kutotumia vifaa vya chanjo kujinufaisha kibiashara na badala yake vitumike kuchanja Mifugo kama ilivyokusudiwa na serikali.

Akizungumza na wafugaji leo Julai 4, 2025 wakati wa Uhamazishaji wa kampeni hiyo katika halmshauri ya Wilaya ya Kilwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Agnes Meena amesema Serikali imeachangia nusu ya gharama kwa chanjo ya Mifugo  kote nchini hivyo wataalam wasitumie vifaa vya chanjo kwa manufaa yao wenyewe bali vitumike kama ilivyokusudiwa na Serikali na  sio  kibiashara.

” Nipende kuwahimiza Viongozi na Watalaam kuhakikisha kuwa hizo chanjo  tulizotoa, kila kitu kitumike kama ilivyopangwa, tusianze biashara, kuku wote watachanjwa bure lakini ng’ombe, mbuzi na Kondoo  Mfugaji utachangia kidogo” amesema Bi. Meena.

Bi. Meena amesema  Kampeni hiyo baada ya kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Simiyu Serikali kupitia wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na halmashauri zimekuwa zikitekeleza kampeni hiyo na kuwahimiza Viongozi na wataalam wa  halmashauri zote nchini kuendeleza Kampeni hiyo.

Aidha,Katibu Mkuu amesisitiza kuwa  sasa ni wakati mwafaka kwa wafugaji kulima malisho ya mifugo na kushirikiana katika uchimbaji wa mabwawa ya maji ya kunyweshea mifugo ili kuendana na ufugaji wa kisasa  na wenye tija.

Kwa upande wake Daktari wa Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Daniel Mdetele amesema baada ya kutambua magonjwa yanayoathiri mifugo na mazao yake katika masoko ya kimataifa, Wizara ilianisha magonjwa kumi na tatu ya kipaumbele na  kuchukua  hatua za kukabiliana nayo ikiwemo utoaji wa chanjo kwa Mifugo yote nchini

” Baada ya kutathimini na kupata magonjwa 13 ya Kipaumbele serikali imechukua hatua za kukabiliana na magonjwa hayo kwa  kuogesha mifugo yote kupitia majosho  yetu lakini pia kwa kutoa chanjo ambayo itaenda kutokomeza magonjwa yanayoathiri mifugo ikiwemo  homa ya mapafu kwa ng’ombe, Sotoka ya Mbuzi na Kondoo na kwa upande wa kuku ugonjwa mdondoo” alisema Dkt. Daniel Mdetele

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa chanjo  Daktari wa Mifugo wa  Wilaya ya Kilwa Dkt. Nyalekwa Mashimo amesema wilaya hiyo ilipokea  chanjo za mdodoo wa kuku 300,000 na hadi Juni 30 mwaka huu jumla ya Kuku elfu thelathini zimechanjwa ikiwa ni sawa na asilimia 10 ya chanjo ya Kuku iliyopokelewa.

Katika hatua nyingine mfugaji Donald Mbuli  wa Kijiji cha Matandu kilichopo katika halmashauri ya Kilwa amesema kwa sasa ana ng’ombe wasiopungua 800 hivyo ujio wa chanjo hiyo utamsaidia  kuikinga mifugo yake na Magonjwa pamoja na kuongeza  thamani ya biashara ya mifugo hiyo.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *