Ilisemwa damu ya mtu haimwagiki bure, hata kabla jogoo hajawika, tayari waliohusika na kuvamiwa na kupigwa kwa Katibu Wa Baraza la Maaskofu (TEC) Padri Charles Kitima, wameanza kujitanabahisha na kuthibitisha nia yao ovu dhidi ya mama Tanzania.

Kundi hilo lililolenga kuzua taharuki kubwa nchini, halikuridhishwa na taarifa fupi iliyotolewa jana na Baraza la Maaskofu kuhusu shambulio la Kitima, ilioonesha ukomavu wa hali ya juu.
Kufuatia kutoridhishwa huko, leo kundi hili limesambaza waraka mrefu wa upotoshaji unaoelekeza Wakatoliki kususia uchaguzi mkuu kwa kutojiandikisha, kutogombea na kutokupiga kura.
Waraka huu wenye chapa za kughushi za TEC, umesheheni maudhui yanayotaka kuchonganisha kanisa na serikali, na kupandikiza mbegu mbaya ya udini kupitia tukio hilo.
Watu hawa walijua wazi kumvamia Padri Kitima kwenye makazi ya maaskofu, siyo tu kutazua taharuki lakini pia kutaibua hasira za Maaskofu, waumini na wananchi wenye mapenzi mema dhidi ya hatua hiyo na hivyo kutumia mwanya huo kupenyeza agenda yao ya kuwagawa watanzania kwa misingi ya dini.
Mungu ni mwema njia yao imekwama, watanzania wamewashtukia, lakini dhamira yao hii ovu imetusaidia jambo moja – kuwabaini upesi watesi hawa wa Dk. Kitima.
Uchunguzi wa tukio hili ukijielekeza vizuri kwenye chanzo cha barua hiyo fake, tutawajua ni kina nani na mipango yao dhidi ya amani na umoja wetu ni ipi.
Watanzania tuendelee kushikamana na kudumisha amani na umoja wetu hasa katika nyakati za majaribu kama hizi.
Mungu Ibariki Tanzania