Jeshi la Polisi mkoani Mtwara linawashikilia watu wawili kutoka Manispaa ya Mtwara Mikindani kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo na kusababisha taharuki kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa huo, SACP Issa Suleiman, watuhumiwa hao wanadaiwa kuzua madai ya kuibiwa sehemu zao za siri na kijana mwenye umri wa miaka 21, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya Morogoro, ambaye alikuwa amekwenda Mtwara kupumzika kwa ndugu zake.
Amesema watuhumiwa waliokamatwa ni Abdallah Fadhili (24), mkazi wa Chuno, na Isihaka Hamisi (26), mkazi wa Likonde, wote wakiwa madereva bodaboda katika manispaa hiyo.
Tukio hilo lilitokea Aprili 5, 2026 majira ya saa 8 mchana katika kata ya Shangani, mtaa wa Veta, ambapo vijana hao walikuwa kijiweni wakisubiri abiria. Inadaiwa kuwa kijana huyo aliwafuata na kumuuliza mmoja wao gharama ya usafiri kutoka Veta hadi Kokobichi.
Kamanda Suleiman amesema ghafla, kabla hata ya kujibiwa, dereva mmoja alianza kupiga kelele akidai ameibiwa sehemu zake za siri. Wakati huo huo, dereva mwingine naye alijiunga na kuanza kupiga kelele akidai hali hiyo hiyo, jambo lililosababisha taharuki na hofu kubwa kwa wananchi waliokuwepo eneo hilo.
Polisi wameonya wananchi kuacha kusambaza taarifa za uongo na kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuvuruga amani, huku wakisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kufanya vitendo kama hivyo.




