Wizara ya Nishati yajivunia jitihada za kuimarisha haki na uwezeshaji wa wanawake

Katika kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Machi 8, 2025, yenye kaulimbiu “Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji,” Wizara ya Nishati imeeleza jinsi inavyoshiriki kikamilifu katika kulinda haki za wanawake, kuimarisha usawa, na kuwawezesha kiuchumi kupitia upatikanaji wa nishati ya umeme na nishati safi ya kupikia.

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, amesema kuwa jitihada hizi ni sehemu ya mpango wa serikali kuhakikisha wanawake wananufaika na maendeleo ya sekta ya nishati, jambo linalochochea usawa wa kijinsia na kuongeza fursa za kiuchumi kwao.

“Tumepeleka umeme kwenye zaidi ya vitongoji 33,000, lakini pia kupitia nishati safi ya kupikia, tumefanikisha usambazaji wa mitungi takribani 402,000, majiko banifu 200,000 pamoja na majiko ya umeme,” amesema Mhe. Kapinga.

Ameeleza kuwa uwekezaji wa serikali katika nishati, hususan nishati safi ya kupikia, unalenga kuboresha maisha ya wanawake, kupunguza mzigo wa kazi za nyumbani, na kuwawezesha kushiriki zaidi katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, Mhe. Kapinga amepongeza hatua zinazochukuliwa katika sekta ya elimu na afya, ambazo zimechangia kuongeza idadi ya wanafunzi wa kike mashuleni na kuboresha huduma za afya kwa wanawake.

“Kupitia Sera ya Elimu Bure, tumeona ongezeko kubwa la wanafunzi wa kike mashuleni. Vilevile, maboresho katika sekta ya afya yamewapa wanawake uhakika wa kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji kutokana na upatikanaji wa matibabu bora,” amesema.

Mhe. Kapinga pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutambuliwa kimataifa kupitia Tuzo ya Goalkeeper, ambayo inatambua mchango wake katika kupunguza vifo vya akina mama wakati wa kujifungua kwa asilimia 80 na kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kwa kila vizazi 1,000.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu yanatoa fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha wanawake wanapata haki, usawa, na fursa sawa katika jamii.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *