Sunday, October 12, 2025
spot_img
HomeHabariWizara ya Nishati yaongoza warsha mpango kabambe matumizi ya gesi asilia

Wizara ya Nishati yaongoza warsha mpango kabambe matumizi ya gesi asilia

Dar es Salaam — Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio, ameongoza wadau wa sekta ya nishati katika warsha ya kutoa maoni kuhusu Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia Nchini (NGUMP), utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka 25 kuanzia sasa.

Warsha hiyo imefanyika leo jijini Dar es Salaam na kuandaliwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), ikiwa na washiriki kutoka serikalini, sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Dkt. Mataragio amesema mpango huo unalenga kubainisha kiasi halisi cha matumizi ya gesi asilia katika sekta mbalimbali ikiwemo viwanda, uzalishaji wa umeme, usafirishaji na matumizi ya nyumbani.

“Mradi huu wa NGUMP utatuwezesha kufahamu kiasi halisi cha matumizi ya gesi asilia katika maeneo mbalimbali, hivyo kurahisisha upangaji wa mgao wa gesi kulingana na mahitaji ya kila sekta,” alisema Dkt. Mataragio.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa mpango huo utasaidia kuimarisha miundombinu ya gesi asilia nchini, pamoja na kutafuta masoko ya gesi ndani na nje ya nchi, jambo litakaloongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.

Aidha, mpango huo utakuwa nyenzo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, ambapo nishati imeainishwa kama kichocheo cha pili kati ya vichocheo vitano vya maendeleo. Pia utachangia katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia pamoja na Sera ya Nishati ya mwaka 2015.

Kwa upande wake, Mhandisi John Bura, mmoja wa washiriki wa warsha hiyo, amesema mpango huo utachochea matumizi ya gesi asilia nchini na kuongeza fursa za uwekezaji.

“Tunaomba Serikali na taasisi za fedha kuharakisha utoaji wa mikopo kwa wawekezaji, hususan wa ndani, wanaotaka kuwekeza katika sekta hii ili huduma ya gesi asilia isambae zaidi na kutoa matokeo chanya kwa taifa,” amesema Bura.

Kukusanya maoni ya wadau kumefanyika baada ya Wizara ya Nishati, kwa kushirikiana na JICA, kukamilisha rasimu ya NGUMP kupitia mradi wa kujenga uwezo katika matumizi na kuongeza uzalishaji wa gesi asilia.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments