Kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania imetangazwa kuwa mtoa huduma rasmi wa mawasiliano na teknolojia ya kisasa katika Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Kupitia huduma zake za Yas na Mixx by Yas, kampuni hiyo itahudumia wafanyabiashara wote katika kituo hicho, ambacho kilifunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 1 Agosti, 2025.
Kituo cha EACLC kinatarajiwa kuwa kitovu kikubwa cha biashara kwa ukanda wa Afrika Mashariki, kikijumuisha zaidi ya maduka 2,000 na miundombinu ya kisasa ya biashara na usafirishaji. Ujenzi wa kituo hicho ulianza mwaka 2022 kama sehemu ya mikakati ya Serikali kukuza uchumi wa ndani na wa kikanda.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi, Afisa Mtendaji Mkuu wa Yas, Pierre Canton Bacara, alisema:
“Yas tunafurahia kuwa sehemu ya mradi huu wa kimkakati unaowapa fursa wafanyabiashara kukuza uchumi wa kidijitali kupitia mawasiliano ya uhakika na teknolojia ya hali ya juu.”

Katika hafla hiyo, Bacara alipata nafasi ya kukutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ambapo walijadiliana kuhusu nafasi ya sekta binafsi katika kusaidia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya taifa.
Kwa upande wake, Rais Samia aliwahimiza vijana kote nchini kutumia fursa zinazotolewa na miradi kama hii badala ya kulaumu kuwa Serikali haiwaoni.
“Tunasema Serikali inatengeneza mazingira kwa vijana – haya ndiyo mazingira yenyewe. Serikali haiwezi kumfikia kila mmoja, lakini tunapoweka miundombinu kama hii, jukumu ni la kwenu kuitumia,” alisema Rais Samia.
Kituo hicho kinatarajiwa kutoa ajira kwa maelfu ya Watanzania na kusaidia kukuza biashara ndogondogo, za kati, na kubwa, huku kampuni ya Yas ikitarajiwa kuwa kichocheo kikuu cha maendeleo ya kidijitali katika eneo hilo.
