Kikosi cha Azam FC kimeanza rasmi mazoezi kujiandaa kwa mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup) dhidi ya AS Maniema Union ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), utakaochezwa Novemba 23, mwaka huu jijini Kinshasa.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Azam, Thabit Zacharia ‘Zaka’, amesema timu itasafiri kuelekea Kinshasa Novemba 19, baada ya kumaliza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC.
“Baada ya mchezo wetu wa ligi dhidi ya Namungo, kikosi kimeanza mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi,” alisema Zaka.
Aliongeza kuwa wachezaji Yahya Zaydi na Feisal Salum (Feitoto) wanaendelea na matibabu baada ya kupata majeraha madogo, na benchi la ufundi lina matumaini watakuwa fiti kabla ya safari hiyo.
“Tunaamini watakuwa tayari kwa mchezo wa kwanza wa kimataifa kwa sababu majeraha yao si makubwa,” alisema Zaka.
Baada ya kumaliza mchezo huo wa kwanza, Azam itarejea nchini kujiandaa na mchezo wa pili wa kundi hilo dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco, utakaopigwa Novemba 30, mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.




