Friday, December 19, 2025
spot_img
HomeBiasharaShirika la Posta Tanzania lazindua promosheni ya "Zigo Ten Ten”

Shirika la Posta Tanzania lazindua promosheni ya “Zigo Ten Ten”

Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Shirika la Posta Tanzania, Ferdinand Kabyemela, ametangaza rasmi kuanza kwa promosheni maalum ya huduma ya EMS iitwayo “Zigo Ten Ten”, inayolenga kurahisisha usafirishaji wa vifurushi nchini kwa gharama nafuu.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Desemba 19,2025 Kabyemela amesema promosheni hiyo inamwezesha mteja kusafirisha mzigo wowote wenye uzito wa kuanzia gramu sifuri hadi kilo moja kwenda sehemu yoyote ndani ya Tanzania kwa gharama ya shilingi 10,000 tu. Huduma hiyo ni sehemu ya EMS (Express Mail Service) inayojulikana kwa uharak­a, uhakika na usalama, huku ubora wake ukiendelea kuwa ule ule kama wa bei za awali.

Ameeleza kuwa promosheni hiyo imeanzishwa mahsusi kwa kipindi cha sikukuu, wakati ambapo wananchi wengi husafirisha zawadi, vifurushi na mizigo mbalimbali kutoka eneo moja kwenda jingine. Vilevile, promosheni hiyo imelenga kuwahudumia wafanyabiashara wadogo na wakubwa wanaosafirisha bidhaa zao kwa wateja waliopo mikoa tofauti.

“Mfanyabiashara wa Kariakoo anaweza kumtumia mteja wake aliyeko Mtwara, au mfanyabiashara wa Mbeya akamtumia mteja wake Arusha kwa gharama nafuu kupitia Zigo Ten Ten,” amesema.

Amefafanua kuwa huduma hiyo inapatikana katika ofisi zote za Posta nchini, ambapo mteja anachotakiwa kufanya ni kufika na mzigo wake, ambao utafungwa vizuri na kusafirishwa kwa haraka hadi unakokusudiwa.

Huduma ya Ufikishaji (Delivery) Bure

Moja ya faida kubwa ya promosheni ya Zigo Ten Ten ni uwepo wa huduma ya delivery, ambapo anayepokea mzigo hatalazimika kufuata ofisini. Atapigiwa simu na mzigo wake utapelekwa moja kwa moja nyumbani, kazini au kwenye eneo lake la biashara bila gharama ya ziada.

Posta ni kwa Wananchi Wote

Kabyemela amesisitiza kuwa Shirika la Posta Tanzania si kwa taasisi za serikali au kampuni pekee, bali ni kwa wananchi wote. Ameeleza kuwa Posta ipo katika halmashauri zote 96 Bara na Visiwani, ikiwa na ofisi katika kila wilaya, na baadhi ya wilaya zikiwa na ofisi zaidi ya moja.

Ameongeza kuwa hatua ya kupunguza gharama kupitia promosheni hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha huduma za umma zinakuwa rafiki na zinawafikia wananchi wa makundi yote ya kipato.

Historia na Uzoefu wa Shirika la Posta

Akijibu swali la mwandishi wa habari, Kabyemela amesema Shirika la Posta lilianzishwa enzi za ukoloni wa Wajerumani, na limeendelea kutoa huduma hadi sasa, likiwa na uzoefu mkubwa, wafanyakazi waadilifu, wazalendo na waaminifu wanaohakikisha mizigo inasafirishwa salama na kwa wakati.

Amebainisha kuwa kupitia EMS, Posta haisafirishi mzigo pekee bali pia inahakikisha unamfikia mlengwa moja kwa moja mlangoni, bila usumbufu wa kufuatilia kwenye vituo vya mabasi au ofisi za wasafirishaji.

Kwa upande wa takwimu, Kabyemela amesema kwa wastani vifurushi zaidi ya 500 hupita kwenye mtandao wa Posta kila siku, idadi inayoweza kuongezeka hadi zaidi ya 1,200 kwa siku wakati wa misimu ya sikukuu.

Kuwalenga Vijana na Teknolojia

Ameeleza kuwa promosheni ya Zigo Ten Ten imelenga pia vijana, hususan wanafunzi wa vyuo, ili kuondokana na changamoto za kufuatilia mizigo kwenye stendi au ofisi za mabasi. Vijana wanaweza kuomba mzigo uwasilishwe moja kwa moja chuoni walipo.

Kabyemela amewahimiza Watanzania wote kuchangamkia promosheni ya Zigo Ten Ten itakayodumu kwa kipindi cha miezi mitatu hadi sita, kama njia ya kupata huduma bora ya EMS kwa gharama nafuu zaidi.

“Posta ipo kwa ajili yako, amesisitiza.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments