Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali yake itaendelea kuongeza nafasi za ajira hasa katika sekta ya afya na utalii, ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira na kuboresha huduma kwa wananchi.
Akizungumza katika moja ya mikutano ya kampeni, Dk. Mwinyi alieleza kuwa ajira mpya zitajikita zaidi kwa wauguzi na wataalamu wa afya, lengo likiwa ni kuhakikisha huduma bora za afya zinafika hadi vijijini. Alibainisha kuwa serikali inaendelea kufanyia kazi changamoto ya upungufu wa watumishi katika sekta ya afya na itaweka kipaumbele kwa wahitimu wa fani mbalimbali za afya.
“Tutahakikisha kila kituo cha afya kina wauguzi na wataalamu wa kutosha. Hili ni jambo la msingi kwa ustawi wa wananchi wetu,” alisema Dk. Mwinyi huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Aidha, aliongeza kuwa sekta ya utalii, ambayo ni nguzo kuu ya uchumi wa Zanzibar, itapewa nafasi kubwa zaidi katika utoaji wa ajira kwa vijana. Alisema serikali yake itaendelea kuvutia uwekezaji katika sekta hiyo sambamba na kutoa mafunzo kwa vijana ili waweze kushiriki kikamilifu katika ajira zitakazozalishwa.
“Kama sekta mama, utalii una mchango mkubwa katika ajira. Tutatoa nafasi zaidi kwa vijana wetu kupata ujuzi na ajira katika maeneo ya hoteli, miongozo ya watalii, huduma za usafiri na maeneo mengine yanayohusiana na sekta hii muhimu,” alisisitiza.
Dk. Mwinyi alisema mpango huu unalenga kupunguza tatizo la ajira kwa vijana na kuimarisha huduma za kijamii katika maeneo yote ya Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa maendeleo wa miaka mitano (2025–2030).




