Mgombea ubunge wa Ludewa, Mkoa wa Njombe, Joseph Kamonga (CCM), ameeleza mafanikio yaliyopatikana wilayani Ludewa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya na miundombinu.
Akizungumza Septemba 22, 2025, katika mkutano wa kampeni wa Mgombea Mwenza wa Urais wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, Kamonga aliipongeza serikali kwa ujenzi wa shule saba za sekondari ikiwemo Njombe Technical School, vituo vya afya vinne, zahanati 22 na nyingine tano zinazojengwa, huku sekta ya afya ikipokea zaidi ya Sh. bilioni 27.7.
Aidha, aliishirikisha serikali changamoto ya barabara wilayani Ludewa, akibainisha kuwa sekta ya miundombinu imepokea Sh. bilioni 180 kupitia TANROADS kwa ujenzi wa barabara muhimu ikiwemo Litoni–Lusitu. Pia alishukuru ulipaji wa fidia ya Sh. bilioni 19 kwa wananchi wa Liganga na upatikanaji wa mbolea ya ruzuku uliosaidia kuongeza mavuno ya mahindi.
Akijibu hoja hizo, Dk. Nchimbi alithibitisha kuwa ujenzi na ukarabati wa barabara muhimu umeingizwa kwenye ilani ya utekelezaji, akibainisha miradi ikiwemo Mkomang’ombe – Mchuchuma, Daraja la Kiwe, Lusitu – Madilu – Lugalala, na Ludewa – Songambele. Alisisitiza kuwa changamoto za barabara zitatatuliwa iwapo wananchi watawachagua tena.




